Habari Mseto

Najivunia makalio yangu, seneta akana kudai huduma ghali za ndege

August 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

SENETA mteule Millicent Omanga aliibua uchangamfu majuzi baada ya ripoti kuibuka kuwa alitaka kubebwa kwenye sehemu zinazoridhisha anaposafiri kwa ndege kutokana na ukubwa wa makalio yake, akidharau viti vya ‘hadhi ya chini, economy class’.

Kulingana na ripoti hizo, ambazo hazikudhibitishwa, seneta huyo aliandikia Tume ya Huduma za Bunge (PSC) akitaka ruhusa ya kusafiri akitumia sehemu ya kibiashara ‘business class’ kwa gharama ya mlipa ushuru, akidai viti vya ndege za humu nchini ni vidogo sana kwa makalio yake.

Lakini baada ya habari hiyo kuchapishwa gazetini, Bi Omanga aliwaka moto, akikana kuwahi kufanya maombi ya aina hiyo.

Kwa maneno mazito, makali na machungu, seneta huyo alikashifu gazeti la Standard kwa kuchapisha taarifa ‘isiyo na msingi’.

“Licha ya Spika na karani wa bunge la seneti kusema kuwa hawana habari kuwa nilifanya ombi la aina hiyo kwa PSC, siamini kuwa gazeti hilo lilitumia ukurasa mzima kuchapisha vitu vidogo badala ya kushughulika na mambo ya umuhimu kwa Wakenya,” akasema Bi Omanga kwa habari aliyotuma.

“Itasaidia kukumbusha gazeti hilo na wengine walio na mawazo machafu kama hayo kuwa ninajivunia shepu yangu na hivyo habari za kupotosha hazitabadili ukweli huo,” seneta huyo akaendelea.

Baada ya mavamizi mengine makali ya maneno kwa waliochapisha, alimalizia kwa kusema kuwa anatilia umuhimu kuwahudumia Wakenya.