Habari Mseto

Nani aliangamiza kikatili nyanya huyu na alitaka nini?

Na GEORGE MUNENE March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA moja katika kijiji cha Kiambawe, Kaunti ya Kirinyaga, inalilia haki baada ya mpendwa wao kuuawa kikatili na mwili wake kutupwa shambani mwake.

Bi Hellen Muthoni, nyanya mwenye umri wa miaka 70, alionekana mara ya mwisho Machi 18 akifanya kazi kwenye shamba lake kabla ya mwili wake kupatikana baadaye umbali wa mita 20 kutoka nyumba alimoishi.

Alikuwa na majeraha shingoni na sehemu nyinginezo mwilini mwake, ishara bayana aliuawa kikatili huku familia na wakazi eneo hilo wakisalia na maswali kuhusu ni nani aliyemuua mjane huyo mkongwe na kwa sababu gani.

Kulingana na familia, Bi Muthoni aliishi maisha yenye utulivu na upweke baada ya mumewe aliyeugua kwa muda mrefu kuaga dunia miaka 10 iliyopita.

Aliuawa katika boma lake na kubururwa shambani ambapo mwili wake ulirushwa shimoni kuficha ushahidi.

Mkondo wa damu ulioelekea kwenye shimo uliashiria marehemu alibururwa mara tu aliposhambuliuwa.

Mwili wake ulipatikana na jamaa wa familia aliyekwenda kumjulia hali alipokosa kuamka asubuhi iliyofuata.

Wanakijiji walishtuka kwa sababu alikuwa mpole na hakuwahi kugombana na yeyote.

“Tulipokosa kumwona Muthoni tulienda nyumbani kwake lakini hatukumpata. Tuliamua kumtafuta shambani mwake na tukashtuka kuona mwili wake uliojeruhiwa ndani ya shimo,” shemeji yake marehemu, Beatrice Wangari, alisema.

“Tunataka waliomuua Muthoni wafichuliwe na kuchukuliwa hatua, kilichomfanyikia jamaa yetu hakikubaliki kamwe,” alisema Bi Wangari, akisimulia walivyotangamana na Bi Muthoni Jumanne, Machi 18, aliyeonekana mchangamfu.

Familia yake ilisema marehemu alijikimu kimaisha kupitia kilimo na hakuwahi kamwe kumtegemea yeyote kupata riziki.

Joyce Gakuhi, alisema alikuwa nyumbani kwake alipopokea habari za kuhuzunisha kuhusu kifo cha shangazi yake.

“Baada ya kufahamishwa, nilisafiri upesi hadi hapo na karibu nizimike nilipoona mwili wake shimoni, tunataka haki itendeke,” alisema.

Mkuu wa Polisi, Kirinyaga, Moses Koskei, alisema walifika upesi kuanzisha uchunguzi tukio hilo liliporipotiwa katika Kituo cha Polisi cha Baricho.

“Waliotekeleza uovu huu ni sharti wasakwe na kushtakiwa, tutawafichua wauaji,” alisema Bw Koskei, akihimiza familia kuwa na subira na kuwahakikishia kuwa haki itatendeka.