Nanok aadhibiwa na ODM kwa kujiunga na Tangatanga
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha ODM kimemvua Gavana wa Turkana Josephat Nanok wadhifa wa Naibu Mwenyeki wa Kitaifa baada ya kuunga mkono mrengo wa Jubilee unaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu, 2022, maarufu kama Tangatanga.
Chama hicho Alhamisi kilitangaza kuwa nafasi ya Bw Nanok imepewa Mbunge wa Loima Bw Jeremiah Lomorukai.
“Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la ODM limeamua kwa kauli moja kumvua Gavana Josephat Nanok wadhifa wake wa Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa. Nafasi hiyo imejazwa na Mbunge wa Loima Mheshimiwa Jeremiah Lomorukai,” chama hicho kikasema kupitia ujumbe kwenye Twitter.
NEC ya ODM inafanya mkutano wa siku mbili kujadili ripoti ya Kamati iliyoongozwa na Bi Catherine Mumo kuhusu mageuzi katika mfumo wa uteuzi wa wagombeaji wa chama hicho.
Mkutano huo unaoongozwa na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga pia unajadili kuamua masuala ambayo ODM itawasilishwa kwa Kamati ya Maridhiano (BBI) inayokusanya maoni kuhusu namna ya kufanikisha mageuzi ya uongozi nchini Kenya.
Bw Nanok ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Magavana (CoG) alinukuliwa mnamo Mei mwaka huu akisema kuwa atamuunga mkono Dkt Ruto kama mgombeaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Alisema ataunga na magavana wengine 14 kutoka Rift Valley kuhakikisha kuwa uongozi wa taifa hili unarejea eneo hilo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.