Naogopa kusimama kizimbani katika mahakama za Kenya, raia wa Uchina asema
Na BENSON MATHEKA
RAIA wa Uchina anayekabiliwa na shtaka la kumpiga mwenzake, Jumanne alifahamisha mahakama kwamba anaogopa yatakayompata akifika kortini.
Kupitia wakili wake, Bw Tang Tian alisema kwamba ana wasiwasi kusimama kizimbani katika mahakama za Kenya.
“Mshukiwa hayuko kortini. Amenieleza kwamba ana wasiwasi kwa sababu hajui yatakayompata akiwa katika korti za Kenya. Tumewasiliana kwa simu lakini ninaomba muda nimshauri,” wakili wake alimfahamisha Hakimu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo.
Mahakama ilifahamishwa kwamba hofu ya mshukiwa ni kwa sababu hana ufasaha wa lugha ya Kiingereza na Kiswahili.
Hata hivyo, Bi Ojoo alisema mahakama ina huduma za wakalimani wa lugha zote na kumtaka mshukiwa kufika kortini kujibu mashtaka.
“Hii sio sababu ya kukosa kufika kortini. Mawakili wanafahamu kwamba tuna wakalimani hata wa lugha zinazozungumzwa katika vijiji vyote China,” alisema Bi Ojoo.
Alikataa ombi la mshukiwa ambaye yuko nje kwa dhamana ya polisi la kupatiwa muda wa wiki moja kujiandaa kujibu shtaka.
“Nitakuwa na mkalimani hapa kortini Alhamisi, mshukiwa anafaa kufika bila kuchelewa,” aliagiza Bi Ojoo.
Tang anakabiliwa na shtaka la kumpiga na kumjeruhi Ku Ming Hung.