Habari Mseto

Ndani kwa kujifanya afisa wa KDF

August 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME ambaye amekuwa akijifanya afisa wa ngazi za juu katika jeshi (KDF) alikamatwa mjini Eldoret na kufikishwa mahakamani.

Benson Makan Boiyo alikamatwa katika kituo cha polisi cha Kapsoya alipotishia kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wa polisi ambao walikuwa wamemwachilia mshukiwa mmoja kwa dhamana ya pesa taslimu.

Kwa mujibu wa polisi ni kwamba Boiyo ambaye alifikika katika kituo hicho kwa kishindo akiendesha gari la kifahari alisababisha vishindo katika kituo hicho kwa kutishia kuwachukulia hatua kali maafisa wa polisi kwa kumwachilia mshukiwa mmoja ambayae alidaiwa kupigana na mke wake.

Boiyo alitaka mshukiwa huyo kuzuiliwa kituoni humo hadi pale angerudi na kutoa amri kuhusu hatua ambayo angepaswa kuchukuliwa.

“Mwanaume huyu alifika katika kituo hiki akijifanya afisa wa ngazi za juu katika kikosi cha jeshi, alijitambulisha kama luteni jenerali wa jeshi, alitishia kutuchukulia hatua kali za kisheria kwa kumwachilia mshukiwa kwa bondi ya polisi,” alisema afisa mkuu wa polisi Eldoret Mashariki Bw Richard Omanga alipokuwa akithibitisha kisa hicho

Bw Omanga alisema maafisa wa polisi waliposhuku uhalali wa afisa huyo walianza kumhoji kabla ya kubaini kuwa kitambulisho cha jeshi alichokuwa nacho kilikuwa bandia.

Hatimaye maafisa hao walimkamata mshukiwa huyo na kumfikisha mahakamani hapo jana.

Mwanaume huyo alikabiliwa na mashtaka ya kujifanya afisa wa jeshi na kuzuia maafisa wa polisi kutekeleza majukumu yao.

Alikana mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu wa Eldoret.

Hakimu alimwachilia kwa dhamana ya pesa taslimu shilingi 20,000.

Kesi hiyo itatajwa leo ili mahakama itoe mwelekeo wake kuhusu kesi hiyo hasa baada ya wakili wa mshtakiwa kudai kuwa mashtaka husika yalikuwa na kasoro hivyo basi yalipaswa kutupiliwa mbali.