Ndani kwa kutumia bintiye kutapeli watalii
Na BRIAN OCHARO
MWANAMKE mmoja kutoka Mtwapa, Kaunti ya Kilifi anachunguzwa kwa madai ya kutumia mwanawe kutafuta riziki kwa raia wa kigeni wanaotembelea eneo hilo. Polisi walisema Bi Sophia Sein Mutaiwua anahusishwa na visa vya utoaji wa taarifa za uongo ili kujinufaisha na masaibu ya wahisani wake
Mwanamke huyo sasa anakabiliwa na shtaka la kutoa taarifa za uongo kwa polisi kuwa mwanawe ambaye ana miaka 17 alichafuliwa na raia wa Zimbabwe. Bi Mutaiwua ambaye pia ni shahidi mkuu katika kesi ya raia wa Uturuki, Bw Elsek Osman, ambayo inaendelea katika mahakama ya Malindi anasemekana kuwa na tabia ya kuwahadaa wageni wasiyomjua kwa kuwasingizia makosa ya kunajisi.
Inadaiwa mshukiwa huyo aliandikisha katika kituo cha polisi cha Mtwapa kuwa Bw Dubbery Bonnie Newman, ambaye anaishi Uingereza alichafua mtoto wake alipokuwa likizoni katika eneo hilo lakini imebainika taarifa hizo ni za uongo.
Lakini madai hayo yalipochunguzwa, polisi waligundua ya kuwa yalikuwa ya uongo na yanalenga kuwaharibia watalii majina. Pia inadaiwa anatumia hila hiyo kama njia ya kujitafutia riziki.
Bi Mutaiwua tayari amefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kutoa taarifa za uongo kwa polisi.
Karatasi ya mashtaka inasema kuwa mshukiwa huyo alielezea Inspekta Andrew Waroi kuwa raia huyo wa Zimbabwe alichafua bintiye, taarifa ambazo alifahamu kuwa ni za uongo.
Kulingana na sharia, iwapo mshukiwa huyo atapatikana na hatia hiyo, anapaswa kufungwa jela maisha sawa sawa na hatia ya kitendo cha kunajisi.
Mahakama iliambiwa kuwa mshukiwa huyo alitembea moja kwa moja hadi katika kituo cha polisi cha Mtwapa kwa nia ya kutoa taarifa za uongo ili ajinufaishe na masaibu ya Bw Newman.
Mshukiwa huyo tayari ametoa ushahidi kwa kesi ya Bw Osman ambayo pia imekumbwa na madai ya taarifa za uongo zinazolenga wageni ambao wamewekeza katika eneo hilo.
Katika kesi hiyo ambayo Bi Mutaiwua na bintiye ndio mashahidi wakuu, mahakama imeambiwa kuwa kesi hiyo haina mlalamishi kwani hakuna taarifa zozote za unajisi zilizoandikishwa katika kituo chochote cha polisi.
Upande wa mashtaka na polisi pia umedhibitisha kwa mahakama kuwa kesi dhidi ya mwekezaji huyo haina nambari ya ripoti (OB) na kuwa taarifa hizo zilipigwa na mtu asiyejulikana.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Bi Alice Mathangaani umesema kesi hiyo haina nambari ya tukio na kuwa hawatawasilisha nambari hiyo.
Hata hivyo, Bi Mutaiwua ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama ya Shanzu, Bw David Odhiambo, alikanusha shtaka ambalo anadaiwa kufanya Septemba 4.
Ripoti za polisi zinasema kuwa mwanamke huyo anachunguzwa kwa visa vya utoaji ripoti za uongo kwa polisi ili kuwahadaa wageni.
Polisi tayari wameanza kumtafuta msichana huyo wa miaka 17, ambaye alitoweka baada ya kupata taarifa kuwa mama yake alitiwa mbaroni kuhusiana na madai dhidi ya Bw Newman.
Bi Mutaiwua aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Kesi hiyo itasikilizwa Septemba 10.