Ndimi za moto zalamba nyumba za familia 30 Kuresoi
NA PETER MBURU
Zaidi ya familia 30 kutoka kata ndogo ya Kongoi katika eneo bunge la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru zinakadiria hasara tele baada ya moto mkubwa kuteketeza nyumba 25 za makazi na biashara usiku wa Jumatatu.
Mairani walisema kuwa moto huo, ambao kiini chake bado hakijabainika ulianza saa tano usiku katika ploti hiyo ambayo imejengwa nyumba za biashara mbele na za kuishi nyuma.
Naibu wa chifu wa eneo hilo Bw George Mayoyo alisema majirani walijaribu kuzima moto huo lakini ukawazidi kutokana na nguvu zake na hali kuwa waligundua wakiwa wamechelewa, na hivyo ukawa umekua mkubwa.
“Hii nip loti ambayo mwenyewe amejenga nyumba za biashara mbele na za watu kuishi nyuma ambapo familia 30 zinaishi. Moto ulikuwa mkubwa na hivyo ukawashinda majirani kuuzima,” akasema Bw Mayoyo.
Afisa huyo aliongeza kuwa familia zilizoadhirika sasa zimetafuta msaada wa mahali pa kuishi kwa majirani, baada ya kuvumilia baridi ya usiku kucha.
Moto huo uliteketeza nyumba zote katika ploti hiyo, huku baadhi ya majirani wakishuku ulichochewa na kufeli kwa nguvu za umeme.
“Bado hatujabaini kiini haswa cha moto huo lakini uchunguzi umeanzishwa. Kuna tetesi kuwa huenda ukawa ulisababishwa na hitilafu za umeme lakini hilo litaamuliwa na mamlaka zitakazochunguza,” akasema Bw Mayoyo.