NDIVYO SIVYO: Tunapaswa kutenga maneno hai na kuwa hai tuwasilianapo
Na ENOCK NYARIKI
BAADHI ya watu wamezoea kusema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuwa uhai.”
Kabla ya kueleza kwa nini kauli hii si sahihi, ni muhimu kueleza sababu mbili ambazo yamkini huwafanya watu kuyakanganya maneno “hai” na “uhai” ambayo yako katika kategoria mbili tofauti.
Kwanza, lugha za kwanza za watu hao haziwezi kuyatofautisha maneno hayo mawili. Pili, neno “hai” haliwezi kutumiwa peke yake kueleza kitendo au hali. Sharti tutumie kitenzi kisaidizi { -wa} kabla ya neno lenyewe. Kwa hivyo, ‘kuwa hai’ ni kinyume cha kufa. Endapo hatutaki kutumia neno hai basi itatubidi tutumie kitenzi ishi.
Waama, wakati mwingine, neno hai halitumiwi kama kinyume cha moja kwa moja cha “kufa” kwa sababu haya ni maneno ambayo yako katika kategoria mbili tofauti. Yammkini hii ndiyo sababu katika baadhi ya misemo, neno “kupona” hutumiwa kama kinyume cha kufa.
Mifano ya misemo hiyo ni: Afua ni mbili, kufa au kupona, Jitahidi kufa kupona na kadhalika.
Hata hivyo, katika misemo hii, neno kupona linaweza pia kuibua dhana ya kunusurika au kusalimika baada ya kupitia misukosuko fulani. Kuna maneno kadha ambayo pia hayawezi kutumiwa pekee kuelezea hali fulani . Maneno hayo sharti yatanguliwe na kitenzi kisaidizi {-wa}. Mfano, tunasema “kuwa mzima”, “kuwa safi” na kadhalika.
Tumedokeza hapa juu kuwa ‘hai’ na ‘uhai’ ni maneno ambayo yako katika kategoria mbili tofauti. Ni muhimu kuifafanua hoja hii kabla ya kuingia kwenye kitovu cha mjadala. Neno ‘hai’ ni kivumishi. Kutokana na kivumishi hiki, tunapata kitenzi huisha. Hata hivyo, kitenzi hiki hakiwezi kutumiwa kwa maana ya ‘kuendelea kuishi’.
Badala yake kina maana ya kurejeshea kiumbe uhai. Uhai ni nomino yenye maana ya hali ya kuwa na uzima. Toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu linaeleza kuwa uhai ni kitu kinachowezesha kiumbe kuishi duniani kwa kuendesha shughuli zake za kiwiliwili.
Turejee kwenye kosa tulilolitanguliza katika mjadala huu: *Ninamshukuru Mungu kwa kuwa uhai. Kasoro katika sentensi hii ipo katika neno ‘uhai’ ambalo katika muktadha huu lina maana sawa na uzima.
Mtu hamshukuru Mungu kwa *kuwa uzima bali humshukuru kwa kuwa na uzima. Kwa hivyo sahihi ni kusema: Ninamshukuru Mungu kwa kuwa hai. Iwapo mzungumzaji atahitaji kulitumia neno uhai kwa maana hiyo hiyo, basi itambidi aseme: Ninamshukuru Mungu kwa kunipa au kunijaalia uhai.
Sentensi: “Ninamshukuru Mungu kwa kuwa na uhai” ijapokuwa inaweza kuibua dhana hiyo hiyo, ina utata wa kimaana kwani inaweza pia kumaanisha “Mungu ndiye anayemiliki uhai” – kauli ambayo ni kweli. Alhasili, ni muhimu kutenga tofauti kati ya maneno uhai na “kuwa hai” tunapowasiliana.