NELLY MATOLO: Ufasaha na sauti yake kwa filamu hutoa nyoka pangoni
Na JOHN KIMWERE
ANAAMINI ana uwezo tosha kuendeleza kipaji chake kama mwigizaji ili kuendelea kuvumisha tasnia ya filamu hapa Kenya na kanda ya Afrika Mashariki kwa jumla.
Bila shaka unaposikiliza kati ya filamu alizoshiriki utapagawishwa na sauti yake tamu tu, huku ukiachia mbali jinsi anavyotamka maneno yake kwa ufasaha.
Hayo tisa. Kumi ni pale utakapokuchukua muda kutazama anayofanya, bila kuongeza ladha yoyote hakika utakubali kwamba ni msanii aliyejaliwa kipaji kweli kando na sura ya kuvutia.
Huyu siyo mwingine bali ni dada, Nelly Ngina Matolo ambaye haichiwi na miondoko ya kimadaha. Mbali na uigizaji pia ni video vixen na mfanyi biashara anayejikuza muuzaji wa viatu na mavazi ya kike katika Kaunti Mombasa.
”Nimeshiriki kazi nyingi tu ambazo tumekuwa tukizipiga bei katika Kaunti ya Mombasa ndani ya miaka minane iliyopita lakini mwaka huu napania kupiga levo nyingine katika uigizaji. Nataka kushiriki muvi zitakazorushwa kupitia baadhi ya runinga za humu nchini,” alisema na kuongeza kwamba ni hatua itakayompiga jeki kutinga levo ya mastaa wa muvi za Nollywood na mataifa mengine barani Afrika.
Hata hivyo alisema analenga kufikia levo yake, Lupita Nyong’o anayezidi kutesa katika muvi za Hollywood. Kisura huyu alisema katika mpango mzima akifanikiwa kupata mtaji ananuia kuanzisha brandi yake siku sijazo ili kusaidia wasanii wanaokuja hasa wa kike ambao mara nyingi hupitia changamoto nyingi mbele ya maprodyuza wa kiume.
Tangu alijiunga na usanii shughuli zote hufanyia mjini Mombasa chini ya makundi mbali mbali ikiwamo Nyenyezi na Starlets. Hivi karibuni chini ya kundi la Starlets anajivunia kutengeneza muvi mbili ikiwamo ’12 Hours’ na ‘Malipo’ walizozalisha kupitia CK Productions.
Kadhalika anasema amefanikiwa kutengeneza filamu ya vichekesho iitwayo Vituko Uswahilini. Kupitia kundi hilo walishirikiana na waigizaji wengi tu wa Bongo Movies wakiwamo Mohamed Haji, Mwanakuu Kombo, Hamisi Omari, Aisha Mata, Haji Ali, Aisha Nondo na Halima Tolo.
Kwa upande wa video vixen anasema amefaulu kushirikishwa kwenye kazi za teke tatu za waimbaji tofauti zikiwa ‘Siku ya Kwanza utunzi wake Pato B,’ ‘Shamba Boy,’ na ‘Redwine.’
Anasema kama ilivyo ada ya wasanii wengi duniani yeye hujifunza mengi kutoka kwa wenzie maana anapenda kuketi na kutazama kazi za waigizaji wa Bongo Movie.
Baadhi yazo zikiwa: Principles of woman ‘Vincent Kigosi,’ Urembo na Scolah ‘Aunty Ezekiel,’ Wonderfull Girl ‘Seth Bosco,’ After Death pia Love and Power ‘Patcho Mwamba,’ Ndoa Yangu ‘Jackline Wolper,’ No point of Return ‘Wema Sepetu,’ Foolish Age ‘Elizabeth Lulu,’ Oprah ‘Irene Uwoya,’ Because of You ‘Rose Ndauka,’ My Angel ‘Yusuph Mlela na Hemed Suleiman.’
Anadokeza kwamba mkasa wa kufiwa na babake mzazi mwaka 2008 ulinipelekea kuacha masomo nikiwa kidato cha tatu shule ya Ribe Girls mjini Mombasa.
Anatoa mwito kwa serikali kuanzisha mkakati mwafaka ili kuinua sekta ya muvi na filamu kuimarika na kutoa nafasi za ajira kwa wasanii wanaoibukia.