Habari Mseto

Ngunjiri amjibu Rais Kenyatta

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Bahati amemjibu Rais Uhuru Kenyatta saa chache baada ya kiongozi wa taifa kumkaripia kwa kile alikitaja ni kupinga handisheki na mpango wa maridhiano (BBI).

Katika taarifa ndefu aliyoichapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Facebook, Bw Ngunjiri amesisitiza kuwa hapingi mpango wa kuleta umoja nchini, lakini anakerwa na wale ambao wanatumia mpango huo kama kisingizio cha kujitakia makuu.

Bw Ngunjiri pia amemlaumu Rais Kenyatta kwa kujihusisha na siasa zaidi alipozuru eneobunge lake badala ya kushughulikia changamoto zinazowakabiliwa wakazi wa eneo hilo.

“Tulimkaribisha Rais kwa upole, lakini mienendo ya mgeni wetu na ujumbe wake vimeibua shauku kuhusu nia yao. Ningependa kumwambia kwamba sipingi handisheki na mpango wa kuleta maridhiano nchini,” akasema Bw Ngunjiri.

Akaongeza: “Kile ambacho ninapinga ni kwamba maridhiano yanayopigiwa debe na Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu sio yenye nia njema. Badala ya kuleta mshikamo wanajenga kuta na mabwawa.”

Mnamo Jumanne Rais Kenyatta alizuru eneobunge la Bahati kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alitumia nafasi hiyo kumkemea Bw Ngunjiri kwa kile alichodai ni mwenendo wa Bw Ngunjiri wa kumtusi kila mara huku akipinga mchakato wa BBI na handisheki.

“Nakuomba Bw Ngunjiri ukome matusi ya kila mara na uniache nifanye kazi yangu huku wewe ukifanya kazi yako kama Mbunge. Lengo langu ni kuleta umoja nchini wala sina haja na siasa zisizo na maana,” akasema Rais Kenyatta.

Lakini Jumatano Bw Ngunjiri amemjibu akisema japo Rais ni kiongozi wa chama chake cha Jubilee, hiyo haina maana kuwa sharti akubaliane na yote anayosema.

“Ningependa kumkumbusha Rais Kenyatta kwamba mojawapo ya kazi yangu ni kutetea masilahi ya wakazi wa Bahati. Na hiyo ndiyo nimekuwa nikifanya. Sijaingilia kazi yake kama Rais wa Kenya. Langu ni kutetea watu wangu na kuhakiki utendakazi wa serikali,” akasema Bw Ngunjiri.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto amekuwa mkosoaji mkubwa wa muafaka kati ya Rais na Bw Odinga.

Kwa mujibu wa Bw Ngunjiri muafaka huo maarufu kama handisheki una nia mbaya ya kuzima ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu, kulingana na makubaliano kati yake na Rais Kenyatta mnamo mwaka 2012 kuelekea uchaguzi mwaka 2013.