• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Ni lawama tu kwenye ripoti ya uchunguzi wa mkasa wa Solai

Ni lawama tu kwenye ripoti ya uchunguzi wa mkasa wa Solai

NA PETER MBURU

Ripoti ya uchunguzi kuhusu mkasa wa bwawa la Patel, Solai kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu imelaumu idara za serikali na wamiliki wa shamba la Patel kwa mkasa ulioua watu 48.

Utepetevu miongoni mwa idara za serikali katika kuhakikisha sheria inafuatwa wakati wa kujenga na kuendesha mabwawa katika shamba hilo, kutojali kwa wamiliki na mameneja wake kuhusu usalama wa wakazi na mapuuza ya malalamishi na tahadhari kuwa kulikuwa na hatari mbele ni baadhi ya sababu kuu zilizotajwa kuchochea mkasa huo.

Aidha, ripoti hiyo kutoka kwa mashirika ya KHRC, Freedom of Information Network (FIN) na Mid Rifts Human Rights network imetaja woga miongoni mwa baadhi ya viongozi na wakazi kwa kuwa wamiliki ni matajiri wenye uhusiano na viongozi wakuu serikalini kuwa sababu iliyozuia kusuluhishwa kwa matatizo ambayo mwishowe yalichangia mkasa huo.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa Juni 29 na mashirika hayo kwa pamoja na ambayo imepewa jina ‘Damned dams, exposing corporate and state impunity in the Solai Tragedy’ (Mabwawa mabovu, kuanika kutojali kwa serikali na mashirika katika mkasa wa Solai) inalaumu serikali kwa kutotimiza wajibu wao wa kulinda vyanzo vya maji na mazingira na wamiliki wa shamba hilo kwa kusababisha mkasa huo.

Ripoti hiyo inadokeza kuwa wakazi wa vijiji vya Energy na Nyakinyua walianza kulalamika kuhusu ukosefu wa maji baada ya mito kuzuiliwa na wamiliki wa shamba hilo miaka ya themanini, ila serikali haikuchukua hatua yoyote.

Ripoti hiyo aidha inarejelea mwaka wa 1980 ambapo mbunge wa zamani wa Subukia Koigi Wa Wamwere aliamsha mjadala bungeni kuhusu masuala ya ukosefu wa maji miongoni mwa wakazi wa vijiji vya Mangu, Bomet, Nyandarua na Ndabibi.

“Mnamo 1980, Bw Wamwere aliamsha suala la kuzuiliwa kwa mito na kampuni ya kahawa ya Patel. Aliyekuwa msaidizi wa waziri wa maji wakati huo alikiri kuwa wakazi wa vijiji hivyo waliteseka wakati wa ukame, lakini akakana kujua kuwa kampuni hiyo ilizuilia mito, baadae aliahidi kuchunguza suala hilo. Haifahamiki ikiwa hatua yoyote iliwahi kuchukuliwa baadae,” ripoti hiyo inasema.

Hii, kulingana na ripoti hiyo ni licha ya malalamishi mengi miongoni mwa wakazi kuwa wangeona nyufa katika baadhi ya mabwawa.

“Mwaka wa 2012, bwawa kubwa zaidi katika shamba hilo lilivunja kingo na mamilioni ya lita ya maji yake yakafululiza kuelekea vijijini, kwa bahati nzuri kulikua na bwawa dogo njiani walikokuwa wakifugwa samaki na ambalo lilisaidia kuzuia maji hayo kuelekea vijijini. Hilo lingesababisha mkasa ambao haujawahi kuonekana,” akasema mkaazi mmoja.

“Uchunguzi wetu ulibaini kujengwa kwa mabwawa wakati wa ukoloni na baada yake kulifanywa kwa njia bovu zaidi. Mengi ya mabwawa, yakiwemo yale ya Solai yalijengwa bila kuhusisha wanajamii na hakukujali maslahi ya jamii jirani ambazo hutegemea kilimo kimaisha,” ripoti hiyo ikasema.

You can share this post!

Hakuna atakayesazwa katika vita dhidi ya ufisadi – PAC

Ombaomba feki akamatwa jijini akijifanya hana mkono

adminleo