Habari Mseto

Ni mimi niliwekea KEMSA presha, Kagwe asema

September 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe amekubali kuwa aliweka presha kwa wasimamizi wa Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (KEMSA) kuhusu ununuzi wa vifaa vya kupambana na Covid-19 lakini akakana madai kuwa alishurutisha kuvunja sheria ya ununuzi.

“Nakubali kwamba niliweka shinikizo kwa Kemsa wakati huo kwa sababu vifaa hivyo nilikuwa vinahitajika kwa dharura kote nchini. Hususan wahudumu wa afya walikuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi. Lakini sikushauri mtu yeyote avunje sheria,” Bw Kagwe asema alipofika mbele ya kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Afya kujibu maswali kuhusu sakata ya Kemsa.

Waziri waliwaambia wanachama wa Kamati hiyo kwamba kama mkuu wa Wizara hiyo ni wajibu wake kutoa mwelekeo wa kisera na ushauri kwa maafisa wanaosimamia mashirika yote huku.

“Katika kufanya hivyo, nyakati zingine huwa najipata kuweka presha kwa maafisa ili tupate matokea tunayotaka. Hata hivyo, sio kazi yangu kumshauri mtu kufanya kosa. Endapo nilimwambia afisa yeye kufanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria angesisitisha nitoe agizo hilo kwa maandishi,” Bw Kagwe akaiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Chege.

Wiki jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kemsa aliyesimamishwa kazi, Jonah Manjari aliambia kikao cha kamati ya seneti kwamba Bw Kagwe ndiye alimwagiza kukiuka sheria za ununuzi wa bidhaa za umma wakati wa kutoa zabuni ya ununuzi wa vifaa vya kinga (PPEs).

“Waziri Kagwe na Katibu wa Wizara Susan Mochache ndio walinipa maagizo kwa njia ya simu na  ujumbe mfupi ninunue kutoka kwa kampuni fulani na kwa bei fulani,” Dkt Manjari akawaambia maseneta wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya wakiongozwa na Seneta wa Transnzoia Michael Mbito.

Lakini Jumatano, Bw Kagwe akasema hivi:  “Ukikosea, usikosee kwa sababu Waziri alikuambia ukosee bali, unakosea kwa sababu ya utepetevu wako na kutojua kutumia sheria za ununuzi.”

Wakati huo huo, Bw Kagwe aliashauri Kemsa kuuza vifaa vya thamani ya Sh7.2 bilioni ambavyo ilinunua kwa bei ghali ili kufidia hasara.

“Hamna haja kwa Kemsa kuhifadhi PPEs katika maghala yake ilhali vifaa hivyo vinahitajika kote nchini. Badala ya kuitisha fedha zingine kutoka kwa serikali itakuwa bora kama wangeuza vifaa hivyo,” akaambia wanachama wa kamati hiyo.