• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 8:55 AM
Niliamuru kufutwa kwa zabuni za Anglo-Leasing – Kinyua

Niliamuru kufutwa kwa zabuni za Anglo-Leasing – Kinyua

Na RICHARD MUNGUTI

MKUU wa Utumishi wa Umma Bw Joseph Kinyua Jumatano alifichua kuwa aliamuru kufutiliwa mbali kwa kandarasi za kashfa ya Anglo-Leasing baada ya kugudua Serikali itapoteza mabilioni ya pesa.

Bw Kinyua alidokeza alimwamuru aliyekuwa mwanasheria mkuu na seneta wa Busia Amos Wako afutilie mbali kandarasi 18 miongoni mwazo ile ya Anglo-Leasing ambapo Serikali ilipoteza zaidi ya Sh3.8bilioni.

Akitoa ushahidi katika kesi inayowakabili ndugu wawili Deepak Kamani , Rashmi Kamani na baba yao Chamanlal Kamani , Bw Kinyua alisema alipogudua kandarasi hazikufanywa kwa njia inayofaa alimtaka aliyekuwa Mwanasheria mkuu Bw Amos Wako kufutilia mbali kandarasi ya kununulia idara ya polisi vifaa vya kisasa vya mawasiliano.

Kandarasi hiyo ilikuwa imetiwa saini na waliokuwa makatibu wakuu Mabw Joseph Magari (hazina kuu ya kitaifa) na Dave Mwangi aliyekuwa akisimamia usalama wa ndani mwaka wa 2003.

Bw Kinyua alisema Bw Wako alifutilia mbali kandarasi kati ya Serikali ya Kenya na kampuni ya InfoTalent yenye makao yake makuu nchini Uswizi.

Na wakati huo huo , Bw Kinyua alisema Serikali ya Kenya iliweka tangazo katika magazeti ya humu nchini na kwenye mitandao ya benki zote humu nchini na pia ng’ambo kuwa kandarasi kuhusu ununuzi wa silaha hizo umepigwa kalamu.

“Kufuatia kufutiliwa mbali kwa kandarasi hiyo kampuni ya InfoTalent ilirudisha Euros 5.2milioni ( sawa na KSh506,965,024) ilizokuwa imepokea kama malipo ya kwanza (arubuni) kupitia kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK),”Bw Kinyua alimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Shahidi huyu barua 47 zilizokuwa zimeandikiwa InfoTalent na Serikali kuwa italipia kandarasi 18 ilizokuwa imetia saini zilifutiliwa mbali.

“Kwa nini uliamuru kandarasi hizi zifutiliwe mbali,” naibu wa mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Nicholas Mutuku alimwuliza Bw Kinyua.

“Kandarasi haikuwa inakubalika kisheria kwa vile hakukuwa na ushindani wa makampuni mengine.InfoTalent iliteuliwa moja kwa moja na kupewa kandarasi hiyo ya kuinunulia idara ya polisi mitambo maalum ya mawasiliano, silaha na hata kujengea idara ya upelelezi wa jinai maabara ya kisasa,” ajibu Bw Kinyua.

Hakimu alieleza sababu ya Bw Wako kufutilia mbali kandarasi hiyo ilikuwa ni kwa sababu wizara ya hazina ilihofia huenda InfoTalent ikadai malipo siku za usoni.

Akijibu maswali kutoka kwa mawakili Kioko Kilukumi , Ahmednassir Abdullahi na Edward Oonge wanaowakilisha washtakiwa hao Deepak , Rashmi, Chamanlal, Mwangi na Bw David Onyonka, Bw Kinyua alisema sheria haikufuatwa kampuni ya InfoTalent ilipoteuliwa kutoa huduma hizo.

You can share this post!

Mume na mke kizimbani kwa kuibia Chase Bank mamilioni

Ushahidi wa Wako na Githu kuhusu Anglo-Leasing wasubiriwa

adminleo