Habari Mseto

Nilifanya ngono nisipatwe na saratani, Askofu Deya ajitetea

June 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

ASKOFU Gilbert Deya aliyezongwa na sakata ya wizi wa watoto amefichua kuwa alishiriki mapenzi nje ya ndoa akiwa nchini Uingereza ili asiathiriwe na saratani ya kibofu (Prostrate cancer).

Kwenye mahojiano na wanahabari, mhubiri huyo alisema alizini alipoishi Uingereza kwa miaka 15, mkewe waliyetalikiana Mary Deya akiwa nchini Kenya.

“Nililazimika kufanya ngono ili nisipate saratani ya kibofu kwani singeishi bila mwanamke,” akasema.

Deya alisema ndoa yake na Mary ilikumbwa na matatizo kwa sababu mke huyo alikataa kumwamini.

“Sababu iliyopelekea mke wangu kunitaliki ni kwamba hakuamini kuwa niliishi peke yangu kwa miaka mingi. Alishuku uaminifu wangu, jambo ambalo ni la kawaida.

“Niliishi London, Uingereza kwa miaka 15. Mimi ni mwanadamu na singeishi bila mwanamuke kwa sababu ningepata kansa ya kibofu,” Deya akasema.

Askofu huyo vile vile aliungama kuwa ana mke mwingine nchini Uingereza.

Deya na Mary wamekuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuendesha biashara ya wizi wa watoto. Inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya mwaka wa 1994 na 2004 katika mtaa wa Mountain View, Nairobi

Mnamo 2017, Deya alirejeshwa nchini Kenya baada ya juhudi zake za kupinga hatua hiyo kugonga mwamba.

Alishtakiwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi lakini akana makosa matano ya wizi wa watoto. Mahakama iliamuru azuliwe rumande katika Gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti.

Mnamo Mei 2018, Deya aliachiliwa huru kwa dhamana ya Sh10 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho na Jaji wa Mahakama Kuu Luka Kimaru.

Awali, mnamo 2014, Mary alifungwa jela kwa miaka mitatu kwa kosa la kuiba mtoto katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta mnamo 2005.

Mwaka 2018, Askofu Deya aliwaambia wanahabari kwamba mkewe ndiye alimsababishia masaibu yote yaliyomwandama.

Alisema alikuwa nchini Uingereza akiendesha huduma yake wakati sakata ya “watoto wa kimiujiza” ilipotokea nchini Kenya.