Habari Mseto

Nilikataa ‘makombo’ na ‘ukabila uliokithiri’ serikalini, asema Munyaka kuhusu uteuzi

Na KITAVI MUTUA November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Mbunge wa Machakos Mjini Dkt Victor Munyaka amesema alikataa wadhifa wa hadhi ya chini aliotunukiwa na Rais William Ruto mwezi jana ili asionekane kuidhinisha mapendeleo na ukabila uliokithiri katika serikali ya Kenya Kwanza.

Dkt Munyaka, mwandani wa karibu wa rais, aliyegeuka mkosoaji wake, alisema uteuzi wake kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji wa Mifugo Nchini (KAGRC) ulikuwa dharau kwa jamii ya Wakamba na juhudi zake za kumfanyia kampeni Ruto kwa miaka 13.

“Baada ya kugawa nyadhifa kubwa kwa watu kutoka jamii yake ya Kalenjin, ingekuwa matusi kwa jamii ya Wakamba endapo ningekubali uteuzi huo. Mimi sio mtu wa kujaza nafasi ndogo zilizosalia serikalini,” Dkt Munyaka akasema.

Alielezea jinsia alivyopoteza kiti chake cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa sababu aliwania kwa tiketi ya chama cha Unitede Democratic Alliance (UDA) ambacho hakikuwa maarufu Ukambani.

“Nilipokaidi matakwa ya jamii yangu, niliadhibiwa debeni kwa sababu ya watu niliokuwa nikiunga mkono. Sikupata kichapo hicho cha kisiasa ili nifidiwe kwa uteuzi unaoonekana kuunga mkono ukabila na mapendeleo,” akasema.

Dkt Munyaka, ambaye ni daktari wa mifugo aliyehudumu kwa mihula mitatu kama Mbunge wa Machakos mjini kuanzia 2007 hadi 2022, hakufichua chama ambacho amehamia baada ya kukatiza uhusiana na UDA inayoongozwa na Rais Ruto.

Alikuwa akiongea wakati wa mazishi ya Queen Mulwa, dadake mfanyabiashara wa Nairobi Kennedy Ngumbau Mulwa katika kijiji cha Mutune eneo bunge la Kitui ya Kati.

Dkt Munyaka alipokataa uteuzi huo, alisema alipata habari kuuhusu kupitia Gazeti Rasmi la Serikali toleo la Oktoba 3, 2024, ishara kwamba hakuwa amejulishwa awali.

Baadaye Dkt Munyaka alisema baada ya kujisaili na kufanya ushauri mpana kwa misingi ya mazingira ya siasa, alichukua uamuzi mgumu wa kukataa uteuzi huo.

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 Mbunge huyo wa zamani alikuwa miongoni mwa wanasiasa wakuu waliokuwa wakiendesha kampeni za chama cha UDA katika eneo la Ukambani.

Alitetea kiti chake cha ubunge wa Machakos Mjini akiwani kwa tiketi ya UDA lakini akabwagwa na Caleb Mule wa chama cha Maendeleo Chap Chap.

Wakati wa hafla hiyo ya mazishi iliyofanyika Jumamosi, Dkt Munyaka aliyeandamana na aliyekuwa Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, alimtaka Rais Ruto kuandaa maombi ya kitaifa ya toba kabla ya mwaka huu kuisha.

“Wakati wa maombi hayo yatakayoshirikisha madhehebu yote Rais Ruto aombe msahama kwa makosa yaliyotendwa.