Habari Mseto

Niliposikia kifo cha Walibora, mikono yangu iliganda – Jack Oyoo Sylvester

April 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Kenya inaendelea kuomboleza kifo cha Profesa Ken Walibora, huku mtangazaji shupavu wa Shirika la Utangazaji Kenya (KBC) Jack Oyoo Sylvester akimkumbuka mwendazake kama mtu aliyependa kabumbu.

Jack almaarufu Kaka Jos, ambaye alimuingiza Walibora katika kutangaza mpira miaka 20 iliyopita alipompeleka uwanjani wa mechi ya Ligi Kuu na kumpatia kipazasauti, ameeleza tovuti ya Taifa Leo anavyomkumbuka Walibora.

“Namkumbuka Walibora kwa mambo mengi tu. Yeye alikuwa mtu mcheshi, muungwana, msiri na mzalendo pamoja na mwanaharakati wa lugha ya Kiswahili. Namchukulia kama johari. Ken hawakuwabeza walalahoi wala walalahai.

Tulifanya naye kazi miongo miwili iliyopita. Alikuja KBC kama mtangazaji wa Kiingereza. Hata hivyo, alionyesha juhudi kubwa katika Kiswahili na alipenda kandanda sana. Alikuwa na kipawa na sauti nyoofu ya kutangaza mpira.

Nakumbuka mechi ya kwanza ambayo tulienda naye uwanjani. Ilikuwa kati ya Kenya Breweries, ambayo ilikuwa nyumbani, na Gor Mahia uwanjani Ruaraka. Nilitangaza dakika 20 za kwanza kisha nikampatia kipazasauti. Nilishangaa kuwa alikuwa anafahamu wachezaji vizuri sana. Alitangaza mechi hiyo kwa lugha sanifu ya Kiswahili.

Walibora alikuwa na sauti nzito ya utangazaji. Mimi nilikuwa wa kwanza kumpa kipazasauti kwa mara ya kwanza KBC. Alitangaza kandanda pia na Ali Salim Manga na marehemu Mohamed Juma Njuguna na Billy Omalla.

Walibora aliwahi kuwa mchezaji. Alikuwa kiungo (nambari sita) katika timu ya Idara ya Uhamiaji. Akiwa mtangazaji, Walibora alishabikia timu tatu za humu nchini. Alizipenda AFC Leopards, Kenya Breweries na Nzoia Sugar. Yeye alipenda klabu ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Nilipopokea habari za kifo chake kwa mshangao. Sikuamini…mikono iliganda. Umetutangulia Prof Ken. Tunakuenzi. Tunakupenda sana. Nenda salama. Mwenyezi Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi.”

Kaka Jos, ambaye alikuwa kipa wa Bonde FC katika kaunti ya Homa Bay miaka ya zanmani kabla ya kufanya kazi na Walibora katika Shirika la Habari la KCB, pia alielezea mshabikiano mkubwa kati yake na marehemu Walibora akisema wote ni waandishi wa vitabu.

Walibora aligongwa na gari kwenye barabara ya Landhies jijini Nairobi mnamo Aprili 10 na kukimbizwa Hospitali Kuu ya Kenyatta alikofariki, ingawa kifo chake kilithibitishwa Aprili 15.

Ripoti zinasema kuwa Walibora anatarajiwa kuzikwa Aprili 22 nyumbani kwake Bonde katika eneobunge la Cherangany.