Habari Mseto

Nisameheni, msinifurushe — nina familia changa, alia Gavana Mutai akiitwa kujitetea Jumatano

Na VITALIS KIMUTAI October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kericho Erick Mutai amewaomba kwa unyenyekevu madiwani wa kaunti hiyo wasimtimue afisini.

Dkt Mutai, ambaye wiki hii atahojiwa kuhusu tuhuma za mienendo mibaya, aliomba msamaha kutoka kwa mahasidi wake wa kisiasa na wakazi wa Kaunti ya Kericho.

Akiongea katika hafla ya mazishi ya diwani wa zamani wa wadi ya Kipchimchim Robert Benard Kipkorir Mutai, Gavana Mutai alikubali kwamba huenda alifanya makosa ndani ya muda wa miaka miwili ambao amedumu afisini lakini akawataka madiwani wafuate mkondo wa maridhiano sio wa kumtimua.

“Kwa madiwani, nakubali kuwa huenda nilifanya makosa kama mwanadamu yeyote, huenda niliwakosea,” Dkt Mutai akasema huku akionekana mwenye hisia nzito.

“Lakini tumefanyakazi pamoja nyakati nzuri na mbaya. Nimesaidia kila moja wenu kibinafsi au kama kikundi bila kupendelea yeyote. Tafadhali naomba mnisamehe,” akaongeza.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Gavana Mutai kuongea mbele ya umma tangu kuwasilishwa kwa hoja ya kumtimua afisini katika Bunge la Kaunti ya Kericho.

Jumatano wiki hii, gavana huyo amepangiwa kufika mbele ya madiwani wa bunge hilo kujitetea kutokana na tuhuma kadhaa dhidi yake.

Wakati wa mazishi hayo, Dkt Mutai alihimiza maridhiano miongoni mwa viongozi, akielezea matumaini kuwa ataendelea kuwahudumia wakazi wa Kericho kwa moyo wake wote.

“Ikiwa ni sharti mnikosoe, fanyeni hivyo, lakini msiniondoe afisini,” gavana aliwaomba waliokuwemo huku akionekana mwenye hisia nzito.

“Mimi ni baba wa watoto watatu wadogo. Wa kwanza yuko katika Gredi 7, wa pili yuko Gredi 3 na mdogo zaidi angali ananyonya. Naomba mnihurumie,” akasema.

Gavana Mutai pia aliomba msamaha kutoka kwa wakazi wa Kericho akiwataka wamsamehe endapo aliwakosea kwa njia yoyote.

Alikariri kuwa uongozi hutoka kwa Mungu na viongozi hutenda makosa.

“Kama viongozi, sisi hubeba msalaba mzito wenye misumari. Baada ya muda tunaweza kuanguka. Huenda nilianguka na kwa hilo, ninawaomba mnisamehe,” akasema.

Hoja ya kumtimua afisini Dkt Mutai imepata uungwaji mkubwa kwani tayari madiwani 37 kati ya 47 wameiidhinisha.

Gavana huyo anakabiliwa na tuhuma za kukiuka katiba, kukiuka Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongoza serikali ambayo imehusika katika vitendo vya ufujaji fedha za umma.

Mbunge wa Ainamoi Benjamin Langat pia alihimiza maridhiano akitoa wito kwa pande zote kusuluhisha tofauti zao kwa manufaa ya wakazi wa Kericho.