Nitatetea kiti changu 2022 – Gavana Mumbi Kamotho
NA SAMMY WAWERU
Naibu Rais Dkt William Ruto amekuwa akihimizwa kuteua mgombea mwenza kutoka eneo la Mlima Kenya ili kufanikisha azma yake kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022, chini ya mrengo tawala wa Jubilee.
Ni mchakato ambao umekuwa ukiendeshwa na baadhi ya wanasiasa katika kundi la Tanga Tanga, na linalomuunga mkono Dkt Ruto.
Gavana Anne Mumbi Kamotho wa Kirinyaga (awali Bi Waiguru), ni mmoja wa viongozi ambao wamekuwa wakipendekezwa.
Mnamo Jumanne pindi tu baada ya mahakama ya juu zaidi nchini kufutilia mbali kesi ya kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua, iliyopinga kuchaguliwa kwa Gavana Kamotho, gavana huyu kwenye maelezo yake alisema huenda akatetea kuhifadhi kiti chake 2022.
“Anapaswa kuruhusu watu wa Kirinyaga waongozwe na viongozi waliowachagua, 2022 akiona anataka kiti tukutane kwa debe,” alisema Gavana Kamotho, akimtaka Martha Karua kuitikia uamuzi wa mahakama ya upeo.
Pia, alimtaka kiongozi huyo kuungana naye katika jitihada za kufanya maendeleo Kirinyaga. “Hili suala aliweke kando, aungane nasi katika kufanya maendeleo. Limekuwa lenye kuchokosha na gharama,” akasema.
Ingawa Naibu Rais Ruto hajatangaza atakayemsaidia kupeperusha bendera kuwania urais 2022, kauli ya gavana huyo ni ishara kuwa shinikizo la wanasiasa wanaomtaka awe mgombea mwenza liko kwenye njia panda.
Kufuatia uamuzi wa mahakama, Mumbi alisema kwa sasa anacholenga ni kufanyia kazi wakazi wa Kirinyaga kwa mujibu wa ahadi zake kabla kuchaguliwa gavana.
Siasa za urithi wa Ikulu 2022 zimekuwa zikisakatwa licha ya salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, Machi mwaka uliopita, maarufu kama Handisheki.
Hata ingawa haijabainika wazi mkataba kati ya viongozi hao, wamekuwa wakikashifu siasa za aina hiyo wakihoji lengo la Handisheki ni kuunganisha taifa. Makundi ya Tanga Tanga na Kieleweke-linaloegemea upande wa Rais na Bw Raila, yamekuwa yakirushiana maneno.