• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Nitateua mwanamke Mkikuyu awe naibu gavana wangu -Sonko

Nitateua mwanamke Mkikuyu awe naibu gavana wangu -Sonko

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amefichua kwamba atachagua mwanamke mtaalamu kutoka jamii ya Wakikuyu kuchukua mahali pa aliyekuwa naibu wake, Bw Polycarp Igathe.

Tamko lake linaashiria naibu wa gavana yuko karibu kujulikana baada ya Bw Igathe kujiuzulu ghafla Januari akidai hakuaminiwa na Bw Sonko kuendesha mipango na usimamizi wa kaunti.

“Ninajua nafasi ya naibu gavana inafaa iende kwa Mkikuyu kwa sababu wengi wao waliniunga mkono, lakini nataka niwe huru kumchagua Mkikuyu nimtakaye.

Tayari nina majina na nitapeana wadhifa huo kwa mwanamke lakini ninataka kwanza nifanye mashauriano na nitashauriana na Rais UhuruKenyatta na naibu wake William Ruto pekee,” akasema kwenye mahojiano katika kituo cha redio.

Ingawa hakutaja majina yaliyo kwenye orodha yake, gavana huyo alisema ameamua naibu wa tatu wa gavana wa Nairobi atakuwa mwanamke, mtaalamu na kutoka jamii ya Wakikuyu ili kurudishia jamii hiyo shukrani kwa kumuunga mkono kwa wingi katika miaka yote ambayo amekuwa kiongozi.

“Nimeshirikiana vyema na Wakikuyu tangu mwaka wa 2010 ambapo walinipigia kura kwa wingi nikiwa Mbunge wa Makadara. Mwaka wa 2013 pia walinipigia kura kuwa seneta na baadaye nikawa gavana. Wao hawana ukabila na kama wangekuwa wakabila, singekuwa gavana,” akasema.

Miongoni mwa wanawake ambao wamekuwa wakisemekana kuwa kwa orodha yake ni aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Bi Margaret Wanjiru, gwiji wa kibiashara, Bi Agnes Kagure, Waziri wa Elimu na Michezo katika Kaunti ya Nairobi, Bi Janet Ouko, aliyekuwa mgombeaji useneta Nairobi, Bi Sussan Silantoi, aliyekuwa mgombeaji wadhifa wa Mbunge Mwakilishi wa Nairobi, Bi Karen Nyamu, na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu, Bi Ann Nyokabi.

Kutokana na matamshi yake, kuna uwezekano mkubwa kuwa atamchagua Bi Kagure au Bi Nyokabi kwani wengine waliobaki hawajafikisha matakwa aliyoyataja.

Bi Kagure, 44, ni mfanyabiashara mashuhuri na mkuu wa kampuni ya bima. Ni miongoni mwa wanawake ambao walifanikiwa kibiashara zaidi nchini kabla kufikisha umri wa miaka 40 na amewahi kutuzwa mara kadhaa kutokana na ufanisi wake.

Kwa upande mwingine, Bi Nyokabi alisomea masuala ya siasa na fedha katika Chuo Kikuu cha York kilicho Toronto, Canada, mbali na kusomea usimamizi wa biashara nchini humo humo.

Mwezi uliopita, iliaminika Bw Sonko aliamua kumchagua Bi Kagure lakini Bi Nyokabi, ambaye ni jamaa ya Rais Kenyatta, akaingia kwenye kinyang’anyiro baadaye huku majina yakipendekezwa na watu wenye ushawishi jijini yakiwemo makundi ya wafanyabiashara, mashirika ya kijamii na wanasiasa.

You can share this post!

Wanafunzi 5700 waliopata C+ wakosa nafasi katika vyuo vikuu

Walimu watisha kugoma wakiendelea kuhamishwa

adminleo