Njaa: Red Cross yaomba msaada wa Wakenya
Na BERNARDINE MUTANU
Shirika la Msalaba Mwekundu linaomba wananchi kulisaidia ili kuwalisha na kuwanywesha wakazi wa Turkana na maeneo mengine yaliyoathiriwa na ukame.
Akihutubia wanahabari Alhamisi, Katibu Mkuu wa KRCS Abbas Gullet alithibitisha kuwa vifo vimeripotiwa katika baadhi ya maeneo kutokana na njaa na mambo mengine.
Alisema alijua habari kuhusiana na kijana aliyeaga dunia Turkana na mwingine aliyekaa siku tatu bila chakula.
“Kulikuwa na kisa cha kijana aliyekaa siku tatu bila chakula na mwingine wa miaka 17 aliyeripotiwa kuaga dunia Turkana. Huenda pia waliaga dunia kwa sababu ya magonjwa mengine ingawa madaktari wanaweza kutuambia,” alisema.
Shirika hilo linalenga kuwalisha wananchi 1.1 milioni walioathiriwa Wajir, Tana River, West Pokot, Tharaka Nithi, Samburu, Nyeri (Kieni), Marsabit, Laikipia, Mandera, Lamu, Kitui, Kilifi, Isiolo, Garissa, Embu, Baringo na Turkana.
Kutokana na hilo, linawaomba Wakenya kulisaidia kuchanga Sh824, 554,720 kuwafaa wananchi wengine katika maeneo yaliyoathiriwa.
“Tayari tumeanza kujiandaa kutoa fedha kwa kaunti nane zilizoathirika zaidi kwa lengo la kuwakimu wakazi wa Turkana, Marsabit, Samburu, Isiolo, Garissa, Wajir, Mandera na Tana River walioathirika,” alisema Dkt Gullet.
Kampeni hiyo itaendelea kwa miezi minne hadi sita kuambatana na maeneo na mvua ya masika inayotarajiwa kuimarisha viwango vya chakula na maji maeneo tofauti.
Idadi ya walioathiriwa na njaa inatarajiwa kwenda juu huku watabiri wa hali ya hewa wakiwa wameonya kuwa mvua hiyo itachelewa.
Kampuni ya Nation Media Group inashirikiana na KRCS kuomba wananchi kuwasaidia wananchi wenzao.