Njagua aonja uhuru baada ya siku 6 seli
Na Richard Munguti
MBUNGE wa Starehe, Charles Kanyi Njagua, Jumatano alionywa dhidi ya kutoa matamshi yanayohatarisha usalama wa wageni wanaofanya kazi na biashara nchini.
Akimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu, Hakimu Mkuu Francis Andayi alisema katiba ya Kenya inawatetea wote wanaoishi nchini wakiwemo wageni.
Hakimu alisema matamshi ya viongozi huathiri uhusiano wa kibalozi wa nchi hii na mataifa ya kigeni pamoja na kuzorotesha uchumi.
Mshtakiwa alikanusha shtaka dhidi yake la kuchochea wananchi dhidi ya wageni, na kuomba aachiliwe kwa dhamana.
Kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu hakupinga ombi hilo lakini akaomba mahakama izingatie usalama wa wageni wanaofanya kazi nchini.
Wakili Dunstan Okatchi akishirikiana na Seneta Irungu Kang’ata, Henry Kurauka na Charles Ogoto waliomba korti imwachilie kwa kiwango cha chini cha dhamana.
Bw Okatchi alimweleza Bw Andayi kuwa Jumanne, Jaji Luka Kimaru alikuwa ameagiza mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana .
Bw Njagua alikuwa ameagizwa na hakimu mkazi Bi Sinkiyian Tobiko azuiliwe kwa siku tatu kuanzia Ijumaa hadi jana ili ahojiwe na polisi, kutokana na matamshi ya uchochezi dhidi ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini.
Bi Tobiko alisema kuwa mbunge huyo yuko na ushawishi mkubwa. Bw Njagua alitiwa nguvuni Alhamisi wiki iliyopita .
Bw Ondimu alimweleza Bi Tobiko kuwa matamshi ya mbunge huyo yanahatarisha maisha ya wakenya wanaoishi ng’ambo.