• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
NMG yakanusha madai kuwa inauzwa

NMG yakanusha madai kuwa inauzwa

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Nation Media Group, Bw Stephen Gitagama akihutubu. Picha/ Maktaba

Na GEORGE SAYAGIE

KAMPUNI ya Nation Media Group imepuuzilia mbali madai kuwa itauzwa kwa serikali ya Jubilee.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Stephen Gitagama, aliomba Wakenya wapuuze uvumi huo ambao umekuwa ukienezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza Jumamosi jioni katika dhifa ya Nation Golf Classic katika klabu ya gofu ya Nakuru, alisema kampuni hiyo inamilikiwa na Wakenya ambao wamenunua hisa na kila mtu ana haki ya kuimiliki.

“Kwa hivyo kama unataka kununua hisa za Nation, nenda tu kwa madalali wa hisa unaotaka lakini kampuni yenyewe haiuzwi,” akasema.

Kulingana naye, lengo la NMG ni kuripoti ukweli wa mambo na kuwakilisha sauti ya wanyonge na itaendelea kutimiza lengo hilo ambalo imeshikilia tangu kampuni ilipoanzishwa mwaka wa 1962.

Bw Gitagama alirejelea msimamo uliotangazwa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Bw Wilfred Kiboro, wiki iliyopita kufuatia madai kwamba kampuni inauzwa kwa familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

Kampuni hiyo ambayo ni kubwa zaidi ya vyombo vya habari katika ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kati inamiliki magazeti, vituo vya redio na televisheni Kenya, Uganda na Tanzania.

Wakati mwanzilishi wa kampuni hiyo, Aga Khan, alipozuru Kenya hivi majuzi, uvumi ulienea zaidi kwamba alikutana na Rais Kenyatta kujadili mipango ya kuuza hisa zake ambazo ndizo nyingi zaidi.

You can share this post!

Raila atakiwa kutangaza ‘Mudavadi Tosha 2022’...

Raila aapa kuhakikisha asasi zote zimefanyiwa mageuzi...

adminleo