NMK yapuuzilia mbali madai huenda Lamu ikaondolewa kutoka orodha ya hifadhi za ukale
Na KALUME KAZUNGU
HALMASHAURI ya Makavazi na Turathi za Kitaifa nchini (NMK) imeondoa hofu iliyopo kwamba huenda mji wa kale wa Lamu ukaondolewa kutoka kwa orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kama eneo linalotambulika kwa kuhifadhi ukale na tamaduni zake ulimwenguni yaani Unesco World Heritage Site.
Katika kikao na wanahabari mjini Lamu, Mkurugenzi wa Masuala ya Hifadhi, Turathi na Makavazi katika NMK, Dkt Purity Kiura amesema Lamu imekuwa ikimulikwa kuhusiana na miradi mbalimbali inayoendelezwa eneo hilo na ambayo inakisiwa huenda ikaathiri tamaduni na ukale wa Lamu, ikiwemo ule wa Bandari ya Lamu (Lapsset.
Dkt Kiura aidha amesema NMK tayari imeandaa makongamano na kujadiliana na kamati husika ya Unesco kuhusu Lamu na kutoa hakikisho kwamba mji wa kale wa Lamu utahifadhiwa ipasavyo licha ya maendeleo ambayo yamekuwa yakitekelezwa eneo hilo kila kuchao.
Amewataka wananchi kuondoa shaka kwamba huenda Lamu ipoteze hadhi yake na kuondolewa katika orodha ya Unesco siku zijazo, akishikilia kuwa mikakati kabambe imewekwa ili kutunza mji huo wa kale na tamaduni zake zisiingiliwe.
Afisa huyo aidha amesema NMK kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Lamu na wadau wengine, pia wako mbioni kuzindua ramani maalum ya uhifadhi na utendakazi itakayosaidia kuendeleza uhifadhi wa mji wa kale wa Lamu kama eneo la utamaduni ulimwenguni.
“Lamu imekuwa ikimulikwa sana na kamati ya utamaduni ya shirika la Unesco ulimwenguni, lakini kumekuwa na wasiwasi na uvumi huenda iondolewe kutoka kwa orodha ya Unesco,” akasema Dkt Kiura.
Akaongeza: “Hivi majuzi kamati ya makadirio ya athari na uhifadhi wa maeneo ya utamaduni ulimwenguni ilizuru hapa Lamu na pia kwenye miradi mikuu inayoendelezwa eneo hili. Tuliwahakikishia kuwa licha ya maendeleo kutekelezwa, serikali kuu imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa maendeleo hayo hayaathiri kwa njia yoyote ustawi na uendelezaji wa mji wa kale wa Lamu kama eneo la kihistoria. Kwa hivyo hakuna la kuhofisha kwamba Lamu yetu itaondolewa kutoka kwa orodha ya Unesco.”
Mji wa kihistoria
Akigusia suala la ujio wa vyombo vya kisasa vya usafiri ndani ya mji wa kale wa Lamu, ikiwemo pikipiki na Tuktuk, Dkt Kiura amesema majadiliano yanaendelea kati ya NMK, serikali ya Kaunti ya Lamu na wadau husika ili kuona kwamba vyombo hivyo havihatarishi mpangilio wa mji huo wa kihistoria.
“Pikipiki na tuktuk zimeathiri matembezi na shughuli za watu hasa kwenye eneo linalokaribiana na ufuo ndani ya kisiwa cha Lamu. Tayari tuko kwenye mazungumzo na serikali ya kaunti na wadau husika ili kuwe na mpangilio maalum wa jinsi vyombo hivyo vitakavyotumika bila kuathiri matembezi na shughuli za watu na mpangilio wa kizamani wa mji huu ambao ni kivutio kikuu cha watalii kwa jumla,” akasema Dkt Kiura.
Lamu ina zaidi ya pikipiki 200 na tuktuk tano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Manispaa ya Lamu, Bw Omar Famau amesema kaunti iko tayari kushirikiana na wadau ili kuwatengea watumiaji wa pikipiki na tuktuk njia zao maalum watakazotumia bila kutatiza wanaotembea kwa miguu mjini.
“Najua pikipiki na tuktuk zimekuwa zikilalamikiwa sana kwa kusababisha ajali za mara kwa mara kwa wenyeji, wageni na hata watalii.Hii ndiyo sababu tunaendeleza majadiliano ili kuibuka na sheria itakayowatengea bodaboda na tuktuk sehemu zao za kuhudumu mbali na ndani ya mji ambako kumetengewa watembeaji wa miguu, punda na mikokoteni. Haya yote ni katika harakati za kuhifadhi mji wetu wa kale usiharibiwe,” akasema Bw Famau.