NMS kuzika miili 166 familia zisipoichukua
Na CHARLES WASONGA
VIJUSI 54 na miili ya watoto 34 walio na umri wa chini ya mwezi mmoja, ni miongoni mwa jumla ya miili 166 ambayo Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) inataka ichukuliwe kutoka mochari tatu za jiji, la sivyo iziike katika kaburi la halaiki.
Katika tangazo lililochapishwa magazetini jana, NMS imetoa makataa ya siku saba kwa umma kuchukua miili hiyo ambayo iko katika hifadhi ya maiti ya City na zile za hospitali za Mbagathi na Mama Lucy Kibaki.
NMS inasema kuwa vijusi hivyo vilitoka mitaa mbalimbali jijini kufuatia uavyaji mimba.“Kulingana na Sheria kuhusu Afya ya Umma, kipengele cha 242 na kanuni za mochari za umma za 1991, umma unaulizwa kutambua na kuchukua miili hiyo ndani ya siku saba. Hiyo isipofanyika NMS itaomba idhini ya kuzika miili hiyo,” likasema tangazo hilo.
Kulingana na tangazo hilo, lililotiwa saini na Mkurugenzi wa Afya Kaunti ya Nairobi, Josephine Kibaru, miili 85 iko katika hifadhi ya City, 13 katika hifadhi ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki na tisa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Mbagathi.
Nyingi za miili hiyo ambayo haijatambuliwa inatoka mitaa kama vile Pangani, Buruburu, Shauri Moyo, Kasarani, Kabete, Ruaraka, Kariobangi, Muthaiga na Langata.
Mingine inatoka maeneo ya mbali na jiji kama Kikuyu, Kiambu, Kitengela, Mai Mahiu, Juja na Ndonyo Sabuk.Kulingana na NMS, baadhi ya sababu za vifo vya watu hao wasiojulikana ni ajali za barabarani, kutumbukia mitoni, kujinyonga, kupigwa risasi na vifo vinavyosababisha na maumbile.
Mnamo Julai mwaka huu Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, aliwashauri wanawake jijini kukoma kuavya mimba na badala yake wajifungue na wamletee watoto hao awalee.Ilani ya jana ni ya tatu kutolewa na NMS mwaka huu katika juhudi zake za kupunguza misongamano ya maiti katika hifadhi ya City na hospitali zake.
Kwa mfano, hifadhi ya maiti ya City ina uwezo wa kusitiri miili 160 pekee na imekuwa ikipokea miili 20 kila siku, kwa wastani. Lakini NMS inasema kuwa wakati huu hifadhi hiyo ina zaidi ya miili 200, hali ambayo inaibua changamoto mbalimbali na sugu, ikiwemo za fkiedha na utunzi wa miili hiyo.