Habari Mseto

Nusu ya familia nchini ni fukara, hupata chini ya Sh10,000 kwa mwezi – Ipsos

October 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

KIWANGO cha umaskini kinazidi kuongezeka nchini licha ya madai ya serikali kuwa hali ya maisha imeimarika.

Utafiti wa hivi punde uliofanywa na kampuni ya Ipsos Synovate umebaini kuwa nusu ya familia za humu nchini ni fukara, kiasi cha kuchuma chini ya Sh10,000 kila mwezi.

Hii ni tofauti na ripoti ya serikali inayoonyesha kuwa imeweka mikakati ya kuimarisha kiwango cha maisha na kupunguza viwango vya umasikini nchini.

Watu wengi hawawezi kumudu bei za bidhaa muhimu kutokana na ukosefu wa kazi huku mapato ya wengi yakiendelea kupungua.

Japo Shirika la Takwimu la Taifa (KNBS) linasema kwamba, hali ya maisha ya Wakenya imebadilika, inakiri kwamba watu zaidi ya 16.4 milioni wantumia chini ya dola moja kwa siku ( Sh100).

Kulingana na mwanauchumi mtajika Robert Shaw, kupungua kwa viwango vya umaskini inavyoeleza serikali, hakumaanishi kuwa maisha ya watu wengi yameimarika.

“Kuna tofauti kubwa kati ya matajiri na masikini. Kuna watu wachache wanaomiliki utajiri mkubwa na mamilioni walio katika umasikini mkubwa sana,” aeleza Bw Shaw.

Kulingana ripoti ya shirika la World Poverty Clock ya mwaka 2018 Kenya ni ya nane ulimwenguni kwa nchi ambazo raia wake wanaishi katika umaskini mkubwa.

Ripoti hiyo inasema asilimia 29 (watu 14.7) ya raia 50 milioni wa Kenya ni maskini na wanatumia chini ya Sh190 kwa siku au Sh5,910 kwa mwezi.

Ukosefu wa sera thabiti

Hii ni licha ya gharama ya maisha kupanda kila mara kutokana na ukame unaokumba sehemu kadha za nchi na ukosefu wa sera thabiti za kiuchumi.

Kwa sasa, watu 6 milioni wanakabiliwa na baa la njaa miezi michache baada ya serikali kujivuta kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

Wadadisi wanasema ukosefu wa usawa, hali ngumu ya maisha na ukosefu wa ajira unaweza kusababisha msukosuko wa kijamii nchini.