Habari MsetoMakala

Nusura mihadarati iniangamize, mwathiriwa asimulia

February 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

DIANA MUTHEU na EVERLINE AKINYI

UTUMIZI wa dawa za kulevya ni mojawapo ya changamoto kubwa inayokumba wakazi wa Pwani.

Kwa miaka 20, Bw Murad Swaleh Breik, 45, alikuwa ameshikwa mateka na dawa za kulevya ambazo alizitumia kwa njia zozote ikiwemo kujidunga, kumeza, kuvuta au kumumunya.

Baada ya kutekwa na uraibu wa mihadarati kwa muda mrefu, Bw Murad aliamua kuvunja pingu hizo na akajipeleka katika kituo cha kurekebisha tabia na maadili alipoona kuwa anachungulia kaburi.

Hata hivyo tayari alikuwa amepoteza muda na vitu vingi vya umuhimu maishani mwake. Kwa mfano, hakuendelea na masomo, alitengana na mke wake, familia yake ilimkana, hakuwa na marafiki, alifungwa jela mara si haba na wengi walitamani afe.

Akisimulia kisa chake katika kituo cha kurekebisha tabia za watu wenye uraibu wa kutumia dawa za kulevya cha Reachout Centre Trust, Old Town- Mombasa, Bw Swaleh alisema kuwa alianza kutumia dawa za kulevya akiwa na umri mdogo sana.

“Katika darasa la nne, tayari nilikuwa nimeanza kuvuta bangi. Pia, niliiba miraa na sigara ya jamaa zangu na kuzitumia. Baada ya kumaliza shule ya msingi niliingilia starehe za kunywa pombe,” Bw Swaleh alisema.

Bw Swaleh alisema kuwa wazazi wake walitengana angali yuko katika shule ya msingi na alipofanya mtihani wa kitaifa hakuweza kuendelea na masomo ya shule ya upili, jambo ambalo lilimsukuma zaidi katika matumizi ya mihadarati akidhani kuwa ingempunguzia mawazo.

“Mara yangu ya kwanza kujaribu heroin ilikua ni mwaka wa 1994 wakati mjombangu alinituma nimnunulie. Nilikutana na vijana wengine wakinunua, tukawa marafiki na hivyo ndivyo nikaanza kutumia heroin. Pia nimewahi kutumia bugizi, ugoro na kokeni” alisema.

Starehe ina gharama na hivyo Swaleh alitumia mbinu zozote kupata pesa ya kufadhili uraibu wake. Alipakia magari, akawa mchuuzi wa saa na alipokuwa mnyonge asiweze kufanya kazi, alianza kuuza mali nyumbani kwake kama vile godoro, nguo na hata vyakula.

“Manamba, kondakta na madereva wengi pia walikuwa wakitumia dawa za kulevya. Dawa hizi zilipatikana kwa urahisi na tulikuwa vijana wengi ambao tulizitumia. Nashukuru Mungu sikuingilia wizi lakini marafiki zangu waliojihusisha na uhalifu waliaga dunia kwa kupigwa na halaiki ya watu ama kwa risasi za maafisa wa polisi,” aliongeza.

Mwaka wa 1997, jamaa zake waliamua kumtafutia usaidizi na walichanga pesa na kumpeleka katika kituo cha kurekebisha tabia huku wakimuahidi kuwa wangemtafutia kazi uarabuni mradi tu amalize programu hiyo.

Hata hivyo, Bw Swaleh hakuweza kudhibiti makali baada ya kuacha kutumia dawa hizo za kulevya na alitoroka kutoka kituo hicho.

“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kwenda kwa kituo kama hicho. Nilipokosa kutumia heroin kwa siku hiyo moja, nilipandwa na wazimu. Sehemu zote za mwili wangu zilikuwa zinauma, hata nywele. Sikuweza kustahimili na hivyo nilitoroka kwenda kutafuta pombe ninywe na heroin, nijidunge,” alisema Swaleh.

Aliongezea kuwa alijaribu kuacha dawa hizo za kulevya, akaenda kwa waganga, jela, maombi lakini wapi.

“Kuna wakati nilikuwa nafanya makosa kimakusudi ili nikamatwe na polisi angalau nipelekwe jela nisitumie dawa hizo za kulevya lakini bado nilishindwa. Nilijitenga na familia yangu na kuanza kulala kwenye mikokoteni hadi makaburini. Watoto wangu walinisihi niache kutumia dawa hizi lakini sikuweza. Iliniuma kuwaona wanalia lakini sikuwa na la kufanya manake uraibu ulikuwa umenisonga,”aliongeza.

Mwaka wa 2013 ulikwa na changamoto mingi na hapo ndipo Bw Swaleh aliamua liwe liwalo ni lazima awache kutumia mihadarati ama akumbane na kifo.

Ilifikia wakati akikosa kutumia mihadarati, alitokwa na damu mdomoni. Kujiokoa alinunua pombe kali, akachanganya na heroin na kujidunga akiwa makaburini ili kama ni kufa, afe hapo.

“Nilijidunga mguuni na kwa bahati mbaya nikapata kidonda ambacho hakikuweza kupona. Nilijua naenda kufa na nilitangatanga ovyo nikiomba pesa na chakula. Nilipopatana na mzee mmoja wa nyumbani, nilimsihi aende aniombe msamaha kwa mamangu na amwambie nilikuwa tayari kurudi nyumbani na kwenda katika kituo cha marekebisho tena,” Bw Swaleh alisema.

Mamake alimhurumia na kumpeleka katika kituo cha Reachout Centre Trust hata ingawa watu wengi hawakuamini kuwa alikuwa ameamua kuacha kutumia mihadarati kabisa.

“Siku ya pili katika kituo hicho, nilikuwa hoi na mngonjwa kabisa kwa sababu sikuwa nimetumia dawa za kulevya. Nilipelekwa hospitalini. Nikiwa nimelazwa nilimuomba Mungu anisaidie nisirudie mihadarati,”aliongeza.

Ilimchukua Swaleh muda wa miezi minne kuweza kusimama na kutembea vizuri bila ya kutumia mihadarati.

“Miezi ya kwanza ilikiwa ngumu. Niliposikia harufu ya dawa za kulevya, nilizitamani lakini kwa kuwa nilikua nimeapa sitazitumia tena, sikuzikaribia,” alisema.

Hata hivyo alipaswa kuendelea na program yake ya mwaka mzima pale kituoni.

“Mimi ni muislamu na mwaka wa 2013 ndio ulikuwa mwaka wangu wa kwanza kufunga kikamilifu katika mwezi wa Ramadhan. Namshukuru Mungu kwa kuwa aliniondolea kiu cha mihadarati,”alisema Bw Swaleh huku akiongeza kuwa alipomaliza programu yake ya marekebisho kupata kazi ilikuwa ni changamoto kubwa.

“Unyanyapaa ndio tatizo kubwa linalowakumba watu waliokuwa wanatumia mihadarati. Ni vigumu kupata ajira mwajiri akigundua iliwahi kutumia dawa za kulevya.”

Kwa bahati nzuri, kituo cha Reachout Centre Trust kilimuajiri kufanya usafi, akapanda cheo na kuwa mjumbe wa ofisi lakini sasa ni mfanyikazi wa kijamii katika kituo hicho.

Sasa, Bw Swaleh na familia yake wako katika hatua ya maridhiano. Wasichana wake wanafurahia na pia aliamua kuoa tena na ana mtoto mchanga.

“Nimejua majukumu yangu na ninajaribu kurejesha ule upendo na ukaribu wa hapo zamani na jamaa zangu,” alisema.

Bw Swaleh alisema wazazi wachukue jukumu la kuzungumza na watoto wao kila wakati ili kutambua pale tabia zao zinapobadilika ili kuzuia wasiathirike na matumizi ya dawa za kulevya.

“Pia kaunti ina jukumu la kusaidia vituo kama hivi kwa kuwa mara nyingi tunategemea misaada kutoka ng’ambo. Pia, ni wajibu wa polisi na mahakama kuhakikisha watu wanaouza dawa hizi za kulevya wamechukuliwa hatua kali ili kukomesha janga hili ambalo limelemaza maendeleo katika jamii yetu,” alisema Bw Swaleh.

Aliongeza kuwa jamii bado haijaelewa sababu watu kutumia dawa za kulevya na pia njia mwafaka ya kupambana na tatizo hilo.

Afisa wa maswala ya sheria katika kituo cha Reachout Centre Trust, Hassan Omar Abdalla alitoa tahadhari kuwa idadi ya watoto chini ya miaka 18 ambao wanatumia mihadarati inaongezeka kila uchao.

Bw Abdalla alisema watoto wanatumia mihadarati kwa viwango vya juu, jambo ambalo wazazi wanafaa kulichunguza kwa umakini.

Alisema katika shughuli zake ameweza kukumbana na watoto zaidi ya 30 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 ambao wanatumia mihadarati kama vile bugizi, wanajidunga heroni na pia kuvuta bangi.

Bw Abdallah alisema watoto hawa wakikamatwa hupelekwa katika magereza ya watoto kwa makosa kama wizi, kusababisha vita ilhali kosa la mihadarati hupuuziliwa mbali.

“Kituo chetu kinahudumia watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watoto hawaruhusiwi kutumia dawa za kupooza makali ya dawa za kulevya. Katika jela za watoto hakuna msaada wowote kuwasaidia kudhibiti makali baada ya wao kuacha kutumia dawa hizo za kulevya na hivyo kuwaacha wakitaabika sana na hata wengine hufariki,” alisema Bw Abdalla.

Afisa huyu alisema kuwa dawa za kulevya kama vile pombe, sigara, miraa, muguka, bangi zinauzwa karibia kila sehemu na watoto wengi huzipata kwa kudanganya wauzaji kuwa wametumwa na wakubwa wao.

“Mtoto akizoea kutumia dawa hizi, basi huweza kujitosa katika uhalifu ilia apate fedha za kufadhili uraibu wake,” aliongeza.

Katika kaunti za pwani haswa Mombasa, kumzuka magenge ya watoto mara kwa mara na migadarati imekuwa ikitajwa kuwa sababu moja inayochangia. Hivyo, kupigana na janga hilo, ni wajibu wa kila mtu.