Habari MsetoSiasa

Nyoro aadhibu mawaziri wa Waititu

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SIMON CIURI

NAIBU Gavana wa Kiambu, Bw James Nyoro ameanza kudhihirisha mamlaka yake kama kaimu kiongozi wa kaunti baada ya kuwapokonya magari ya serikali mawaziri wawili ambao ni wandani wa Gavana Ferdinand Waititu.

Mawaziri wa serikali ya kaunti waliopokonywa magari ni Bi Juliet Kimemia (Barabara, Usafiri, Ujenzi na Kawi) na Bw Kigo Njenga (Fedha na Mipango) ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Gatundu Kaskazini.

Bw Nyoro jana alisema kuwa aliagiza wawili hao wapokonywe magari ya serikali ya kaunti na madereva wao wapewe majukumu mengine. Alisema mawaziri hao wamekuwa wakijihusisha na siasa badala ya kuwatumikia wakazi wa Kiambu.

“Ni kweli kwamba niliagiza wawili hao wapokonywe magari kwa sababu wamekuwa wakitumia muda mwingi katika siasa badala ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Wamekuwa wakitumiwa na wafadhili wao kutatiza miradi ya maendeleo. Watarudishiwa magari yao endapo wataachana na siasa na badala yake wawafanyie kazi wakazi wa Kiambu,” akasema Bw Nyoro.

Alisema alichukua hatua hiyo kulingana na agizo la Rais Uhuru Kenyatta aliyepiga marufuku siasa za mapema.

Alisema kuwa mawaziri hao wanatumiwa na Gavana Waititu kutatiza shughuli za baraza la mawaziri. Aliwataja mawaziri hao kama ‘adui wa maendeleo’.

Bw Kigo na Bi Kimemia waliambia Taifa Leo kuwa tayari wamepokonywa magari na madereva wao wamepewa majukumu mengine.

“Gari la serikali ya kaunti ambalo huwa ninatumia lilitwaliwa Ijumaa. Nyoro anahofia kwamba huenda nikambwaga endapo nitashindana naye katika kinyang’anyiro cha ugavana 2022. Hivyo analenga kunidhalilisha kwa kuninyang’anya gari,” akadai Bw Kigo.

Bw Kigo Njenga aliyepoteza kiti chake cha ubunge katika uchaguzi wa 2017, ni mwandani wa Gavana Waititu.

Bi Kimemia aliwania kiti cha useneta wa Kiambu katika uchaguzi uliopita lakini akashindwa.

“Nilipokonywa gari langu rasmi Ijumaa na sijawahi kutatiza miradi ya maendeleo kama inavyodaiwa,” akasema Bi Kimemia.

Waziri wa Vijana, Bw Karung’o wa Thangwa pia amekuwa akishutumiwa na Kaimu Gavana Nyoro kwa madai ya kutumiwa na Bw Waititu kutatiza miradi.

“Nimempa moja ya magari yangu rasmi mwenzangu Waziri wa Fedha Kigo Njenga aliyepokonywa gari lake katika hali ya kutatanisha,” akasema Bw Thang’wa kupitia mtandao wa Twitter.

Bw Thangwa amekuwa akisisitiza kuwa hamtambui Bw Nyoro kama kiongozi wa kaunti kwani hana mamlaka ya kuajiri au kutimua wafanyakazi wa kaunti.

“Mamlaka hayo yamepewa gavana. Nyoro ni naibu gavana asiyekuwa na majukumu au mamlaka yoyote,” akasema.

Ijumaa, Bw Nyoro, kupitia notisi katika Gazeti Rasmi la Serikali, alitangaza kumhamisha Bw Kigo kutoka wizara ya Fedha hadi wizara ya Biashara na Utalii. Nafasi yake ilitwaliwa na Bw Wilson Mburu Kangethe.