Nyumba 50 zateketea Mukuru-Kaiyaba
Na SAMMY KIMATU
ZAIDI ya watu 100 walikesha nje penye baridi baada ya nyumba 50 kuteketea katika eneo la Dallas kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba mwishoni mwa juma.
Moto huo ulianza katika nyumba moja baada ya vijana wawili kuzozana na kisha ukachochewa na upepo mkali.
Gari mbili za kuzima moto kutoka Kuanti ya Nairobi fauka ya kuwasili mtaani hazikufaulu kufika kwenye eneo la mkasa kufuatia ukosefu wa njia baada ya barabara kunyakuliwa.
Bi Monicah Juma, 43, ambaye kadhalika ni mhuduu jamii wa kujitolea alisema aliarifiwa kuhusu mkasa huo na mtoto lakini alipowasili akakuta nyumba yake imeteketea. Hakuokoa chochote.
Bw Onesmus Kalei, mkazi m,taani humo na mmiliki wa nyumba kwenye eneo la kisa alisema vijana walipigana kwa ukucha na jino wakitumia maji ya mifereji huku wengine wakibomoa nyumba moto usienee Zaidi.
Aliwaomba wakazi kubomoa vibanda na nyumba ikiwa watanusuru maisha yao na mali ndiposa njia ya dharura ipatikane.
Huku shule zikiwa zimefungwa, nao watoto walifurika kutafuta vyuma kuukuu na vingine vya dhamana kwao.
“Huu mkasa ni wa saba kutokea mtaani huo mwaka huu pekee,” Bw Kalei akaambia wanahabari.