Habari MsetoSiasa

Obado awaumbua maseneta kwa kumwanika Waititu

May 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

GAVANA wa Migori Okoth Obado Jumatatu alifika mbele ya Kamati ya Seneti Kuhusu Uhasibu akiwa amejipanga kukabiliana nayo vilivyo kuhusu jinsi kaunti yake ilitumia pesa za umma, baada ya kisa ambapo mwenzake wa Kiambu Ferdinand Waititu alikaangwa wiki mbili zilizopita.

Punde tu alipopewa fursa ya kutoa maneno ya kufungua kikao mbele ya kamati hiyo, Bw Obado alianza kwa kumvamia mwenyekiti wa kamati Moses Kajwang kuwa hakuwa na usawa akisema alimvamia katika hafla ya umma wikendi iliyopita na akawalaumu maseneta kuwa wanawaita magavana ili kuwaaibisha badala ya kukagua kuhusu jinsi pesa za umma zimetumiwa ipasavyo.

Gavana huyo aidha alimtahadharisha seneta wa kaunti yake Ochillo Ayacko kuwa endapo angethubutu kumvamia alikuwa tayari kumkabili, akiibua hisia kuwa alikuwa amefika akiwa tayari kwa lolote.

“Nyinyi maseneta mnafaa kuwa mkiunga mkono ugatuzi ili kuufanikisha, msiwe mkiwaona magavana kama watu fisadi wasioweza kusimamia chochote. Mwenzangu Gavana wa Kiambu mlimhangaisha hapa hadi nikamhurumia sana, hiyo haifai,” akaanza Bw Obado.

Gavana huyo aliendelea “Hata nilipokuwa nikijiandaa kuja hapa, kwenye akili nilikuwa nikishangaa ikiwa pia mimi mtaniambia kuwa kuna matumizi nimefanya yasiyo ya kawaida. Tuwache kuwahadaa Wakenya kuwa magavana peke yao ndio fisadi.”

Lakini matamshi yake yalimweka katika hali ya makabiliano na maseneta, ambao walishikilia kauli yao kuwa sharti wakague matumizi yote ya kaunti.

“Maafisa wa umma ambao hawaheshimu kiapo cha kazi na kufanya kazi inavyofaa wanafaa kuaibishwa,” akasema seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi.

Maneno yake yaliibua mjadala wa muda na maseneta ambao ulichelewesha kidogo mjadala halisi kuhusu ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Pesa za Umma, kuhusu jinsi Kaunti ya Migori ilitumia pesa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu ilisema kuwa afisi hiyo haikutoa maoni yoyote kuhusu jisni Kaunti ya Migori ilitumia pesa 2017/18, kutokana na kisa cha moto mnamo Septemba 24, 2018 ambapo ilidaiwa kuwa nakala za kuthibitisha jinsi pesa zilitumika ziliteketea, wakati moto ulitokea katika majumba mawili.

Kutokana na moto huo, Mkaguzi Mkuu hangeweza kubaini ikiwa pesa za umma zilitumiwa ifaavyo na kisheria

Maseneta, hata hivyo walikuwa na maswali tele kuhusu ni kwanini kaunti hiyo haikuwa na nakala za ziada za kukinga kutokana na hali ya aina hiyo, lakini Gavana Obado akisema kuwa yuko tayari kuthibitisha jinsi pesa hizo za miezi mitatu (kati ya Julai 1 na Septemba 24 wakati moto ulitokea), ambazo ni zaidi ya Sh1.5 bilioni zilitumika.

“Tunaweza kuthibitisha jinsi kila peni ilitumika kwani hakuna pesa zilizotumiwa isivyofaa, yalikuwa mambo ya kawaida kama kulipa mishahara na kulipa wakandarasi,” akasema Bw Obado.

Kamati hiyo ilimpa siku saba kuwasilisha ushahidi kuhusu jinsi alitumia pesa hizo.