Habari Mseto

ODM yaendelea kulalama kuhusu kupewa fedha kidogo

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimefichua kinahitaji Sh50 milioni kuendesha shughuli za afisi za matawi yake kote nchini kila mwezi, ilhali hakina pesa hizo.

Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna amesema kinakabiliwa na changamoto za kifedha kiasi kwamba imekuwa vigumu kwake kupata fedha hizo za matumizi.

“Tunapaswa kupata Sh1 bilioni kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa lakini huwa tunapokea Sh120 milioni kwa mwezi ambazo hazitoshi kugharamia mahitaji yetu,” amewaambia wanahabari Alhamisi asubuhi jijini Nairobi.

Akaongeza: “Kiasi hiki ni sawa na tone kwenye maji na ni fedha ambazo haziwezi kutosha. Tunanyimwa fedha ambazo ni stahili yetu. Hatujui ni kwa nini.”

Hujuma

Bila kutoa ithibati, Bw Sifuna amedai kuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich anahujumu shughuli za upinzani.

“Wakati huu tunadai serikali Sh5 bilioni tangu mwaka wa 2013. Tunahitaji fedha hizi kuendesha shughuli ya elimu ya urais na kuendesha shughuli za afisi zetu,” akaeleza.

Kulingana na Katiba, vyama vya kisiasa hutengewa asilimia 0.3 ya bajeti ya kitaifa, lakini mara nyingi, vyama hivyo hudai kuwa vimekuwa vikipokewa kiasi kidogo cha fedha kuliko kila ambacho serikali huwatengea kila mwaka.

Mnamo mwaka wa 2016, ODM iliwasilisha kesi kortini ikitaka Hazina ya Kitaifa ilazimishwe kuzingatia kanuni ya vyama kuwa vinatengewa asilimia 0.3 ya bajeti ya kitaifa.

Lakini sheria hiyo inasema kuwa ni vyama vilivyopata angalau asilimia tano ya kura zote za urais ndivyo vinapaswa kupokea pesa hizo.

Hii ndiyo maana vyama vya vidogo kama vyama tanzu katika muungano wa NASA vilivyounga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga vimekuwa vikilalamika kuwa chama hicho hakijavigawia pesa kinachopokea kutoka kwa serikali.

Vyama hivyo ni Ford Kenya, Amani National Congress (ANC) na Wiper.