Habari MsetoSiasa

Ole Lenku awaonya wanaochochea ghasia za kikabila

January 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kajiado Bw Joseph Ole Lenku ameomba maafisa wa usalama kuwachunguza viongozi kutoka kaunti hiyo aliodai wanachochea wakazi kuzua chuki na ghasia za kikabila.

Bw Lenku aliwataka wakazi kuwapuuza viongozi hao na kuishi kwa amani akisema wanalenga kutimiza maslahi ya kisiasa.

“Kataeni kudaganywa na watu wanaowachochea kuzua ghasia. Wanachotaka watu hao ni kutumia raia wasio na hatia kuzua chuki za kikabila ili watimize maslahi yao ya kisiasa. Hatutaki hali kama hiyo hapa Kajiado, tuishi kwa amani,” alisema Bw Lenku.

Akizungumza alipojumuika na wakazi wa Kitengela kusherehekea mwaka mpya, Gavana Lenku alisema baada ya watu wanaomezea mate viti vya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 wamekuwa wakizunguka kaunti hiyo wakieneza chuki za kikabila.

“Kuweni macho na msikubali kudaganywa ili muangukie mitego ya watu hao ambao lengo lao ni kuzua ghasia kutimiza malengo yao ya kisiasa,” alisema.

Alipongeza juhudi za serikali za kupiga vita ufisadi na akasema vita hivyo vinapaswa kuendelea. Bw Lenku alisema serikali yake inashughulikia uhaba wa maji unaokumba mji wa Kajiado na vitongoji vyake.