• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Onyo kali kwa wanaogeuza karantini kuwa maeneo ya burudani

Onyo kali kwa wanaogeuza karantini kuwa maeneo ya burudani

Na MARY WANGARI

WAKENYA walio katika karantini kuhusiana na ugonjwa wa Covid-19, huenda wakalazimika kukaa katika vituo hivyo kwa muda mrefu zaidi, huku ikibainika kuwa baadhi yao wamegeuza vituo hivyo kuwa sehemu za burudani.

Akizungumza Jumatano katika kituo kimojawapo cha redio, Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna aliwatahadharisha watu waliotengwa dhidi ya kutangamana akisema wanajiweka katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

“Wakenya walio karantini wanazidi kutangamana na hata kushiriki burudani. Kadri wanavyotangamana ndivyo watakavyoendelea kukaa katika vituo hivyo kwa kuwa hujui ni nani ana virusi vya corona,” alieleza Kanali Oguna.

Akifafanua kuhusu tofauti kati ya vituo vya karantini na vituo vya wagonjwa waliotengwa, afisa huyo wa serikali alieleza kwamba baadhi ya watu walio karantini wamelazimika kukaa katika vituo hivyo hata baada ya kukamilisha siku 14.

“Vituo vya karantini vinahusisha watu wanaoshukiwa kuambukizwa virusi vya corona lakini bado hawajafanyiwa vipimo ili kuthibitishwa. Wengi wao ni watu waliotangamana na mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na Covid-19 baada ya vipimo,” akasema.

“Kila kunapopatikana mtu aliye na virusi hivyo, waliomo itabidi waendelee kukaa karantini kwa siku 14 zaidi hata kama walikuwa wamemaliza muda huo huku wakiangaziwa ili kuhakikisha hali yao ni salama kabla ya kuruhusiwa kujumuika na umma,” alifafanua.

Vituo vya wagonjwa waliotengwa kwa upande mwingine, vinahusisha wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Covid-19 baada ya kufanyiwa vipimo.

Aidha, Kanali Oguna alisisitiza umuhimu wa watu walio karantini kuzingatia vilevile masharti ya kudumisha umbali unaoruhusiwa wa kutangamana kijamii akisema wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

“Ikiwa umma ulio nje unaagizwa kujitenga, je, ni vipi zaidi walio katika karantini watahitajika kujiepusha kutangamana baina yao?” alihoji Bw Oguna.

Kauli yake imejiri siku tatu tu baada ya Wizara ya Afya nchini kuwaongeza Wakenya na raia wa kigeni siku 14 zaidi katika karantini baada ya kuibuka kwamba walikuwa wakitoka vituo hivyo kisiri na kwenda kuvinjari katika vituo vya burudani.

Akitoa amri hiyo, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alieleza kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa dhidi ya watu waliotengwa katika kituo cha Kenya School of Government, ilidhamiriwa kuzuia maambukizi zaidi.

“Kuna watu wanaoendelea kuburudika katika vituo vya karantini. Hii ni kinyume na kila kanuni tuliyotoa. Katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi kutoka kwa waliowekwa karantini kwa lazima, tumeagiza vikosi vyetu vya matibabu kuongeza muda wa walio katika vituo hivyo ambao tunaamini wanahitaji siku 14 zaidi ikizingatiwa watu waliotagusana nao wamepatikana na virusi hivyo,” alisema.

Kuhusu madai kuwa takwimu zinazotolewa na serikali kuhusu idadi ya maambukizi na vifo kutokana na Covid-19 haziashirii uhalisia wa kutosha, Msemaji huyo wa serikali alikanusha madai hayo kama porojo zisizokuwa na msingi.

“Hakuna kinachofichwa na serikali kuhusu maambukizi haya. Kwa wanaotoa madai hayo, serikali itafaidika vipi kwa kuficha takwimu hizo au kwa kutoa takwimu za uongo. Takwimu zinazotolewa ndio uhalisia uliopo,” alieleza.

Isitoshe, aliwahimiza Wakenya walio na uwezo wa kununua barakoa kufanya hivyo ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya Covid-19, huku serikali ikijitahidi kusambaza vifaa hivyo kwa wananchi.

You can share this post!

Makahaba wataka wawekwe kwa orodha ya wanaotoa huduma...

Serikali yatakiwa kuwapa raia pesa badala ya chakula

adminleo