Orengo ataka Dkt Ruto atoe maelezo kuhusu sakata inayomkabili Echesa
Na CHARLES WASONGA
SENETA wa Kaunti ya Siaya James Orengo amemtaka Naibu Rais William Ruto kutoa maelezo kuhusu anayoyafahamu kuhusiana na madai kwamba aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa aliwalaghai wafanyabiashara wa kigeni kuhusu zabuni feki ya Sh39.5 afisini mwake.
Akiongea Jumamosi katika hafla ya mazishi katika eneobunge la Matayos, Kaunti ya Busia, Orengo alisema madai hayo yanatoa picha mbaya ya afisi ya Naibu Rais na kuisawiri kama kitovu cha ufisadi.
“Inasikitisha kuwa afisi ya Naibu Rais imegeuzwa kuwa eneo la tukio la uhalifu. Iweje kwamba watu wanaweza kuingia afisini mwake wakijifanya maafisa wakuu wa jeshi? Hii inashangaza,” Bw Orengo akasema.
Akaongeza: “Tunataka maelezo kutoka kwa Naibu Rais kuhusu madai hayo ambayo yanashusha hadhi ya afisi hiyo yenye heshima na taadhima.”
Seneta huyo wa Siaya alisema hayo saa chache baada ya Dkt Ruto kujitenga na madai yanayomzingira Echesa, akisema wanaomhusisha na sakata hiyo ni wapinzani wake wa kisiasa.
“Wanaosambaza madai hayo ni wapinzani wangu ambao wamepanga njama ya kumharibia sifa. Hata wajinga (ambao ni haba zaidi nchini) wanaweza kuona. Subiri uone mahala ambapo madai haya yataishia. Washindwe. Mwandamane walaghai na mniache nihudumie taifa,” akasema kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
Alisema hayo baada ya gazeti moja la Jumamosi kumrejelea Bw Echesa kama mwandani wake na kudai kuwa aliendesha ulaghai huo ndani ya afisi ya Dkt Ruto katika jumba la Harambee Annex.
Echesa, na watu wengine watatu, walikamatwa Alhamisi kwa madai kuwa waliwalaghai wafanyabiashara wa kigeni Sh115 milioni wakiahidi kuwasaidia kupata zabuni ya kuuzia Wizara ya Ulinzi silaha na vifaa vya usalama vya thamani ya Sh39.5 bilioni.
Vilevile, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walidai kuwa Echesa na wenzake walighushi stakabadhi na sahihi ya Waziri wa Ulinzi Monica Juma kufanikisha ulaghai huo.
Washukiwa hao wanazuiliwa rumande baada ya kufikishwa katika mahakama ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) ambapo walisomewa mashtaka.