Habari MsetoSiasa

Passaris kuhusisha DCI katika mvutano na Sonko

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA COLLINS OMULO

MBUNGE Mwakilishi wa Kike, Kaunti ya Nairobi Esther Passaris jana alisema atahusisha asasi za uchunguzi kutegua kitendawili kuhusiana na madai mazito yaliyotolewa na Gavana wa Nairobi Mike Sonko kumhusu.

Mwanasiasa huyo alisema atafika katika ofisi za DCI, EACC na NCIC ili kusafisha jina lake kutokana na madai kwamba alitaka alipwe marurupu ya usafiri mara mbili; kutoka kwa serikali ya kaunti na Bunge la Kitaifa.

Bi Passaris alishikilia kwamba madai yalitotolewa na gavana ni ya uongo na hayana msingi huku akiapa kwamba hii itakuwa mara ya mwisho maadili yake yatatiliwa shaka kupitia uongo, matamshi yaliyoonekana kumlenga Bw Sonko.

Akizungumza katika uwanja wa JKIA baada ya kurejea nchini kutoka Canada alikohudhuria kongamano la wanawake, Bi Passaris alifafanua kwamba madai yote yaliyotolewa na Bw Sonko wakati wa mahojiano kwenye runinga ya Citizen yalikuwa uongo na hayana msingi.

“Ni kazi rahisi kwa DCI na EACC kuyachunguza madai yote dhidi yangu na kubaini nani msema kweli. Nitafika katika afisi za DCI, EACC, NCIC na Tume ya Jinsia baada ya kushauriana na mawakili wangu na asasi za serikali

“Hili suala halitaisha vivi hivi na hii ni mara ya mwisho kwa mtu yeyote kutilia shaka maadili yangu kwa kueneza uongo,” akasema mbunge huyo wa chama cha ODM.

Vile vile alimtaka Bw Sonko kuwasilisha ushahidi kutokana na madai aliitisha malipo ya marupurupu ya usafiri mara mbili kuhusiana na kongamano alilorejelea.

“Tuna sheria katika taifa hili na nitatumia kila sheria kupitia mwongozo wa katiba kuhakikisha hii ni mara ya mwisho kwa mtu yeyote kutumia uongo kuangusha wanawake au viongozi wanawake,” akaongeza Bi Passaris.

Aidha alipuuzilia mbali madai kwamba aliamwalika Bw Sonko kwenye chumba chake katika hoteli moja mjini Nairobi, akisema ni gavana huyo alimpigia simu akitaka kujua kama alikuwa amefika hotelini humo kuhudhuria warsha ya wabunge.

“Gavana alinipigia simu kujua kama nilikuwa kwenye warsha hiyo kwa sababu kulikuwa na hofu wabunge wa ODM wangeisusia. Nilimjibu nilikuwa kwenye hafla hiyo na ningependa uongozi wa hoteli hiyo kutoa maelezo yote kuhusu uwepo wangu humo,” akaendelea Bi Passaris.

Kiongozi huyo pia alikanusha kwamba wakati wa sherehe za Madaraka alilalamika kwamba gavana hapokei simu zake, akisema hakutamka jambo kama hilo wala hajui jinsi suala hilo lilivyochipuka.