Habari Mseto

Pasta alitunga mimba mwanafunzi wa darasa la 7, DNA yaonyesha

September 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

UCHUNGUZI wa vinasaba (DNA) umeonyesha kuwa mhubiri mmoja katika Kaunti ya Kitui alimtia mimba mwanafunzi wa darasa la saba.

Uchunguzi huo ulioamrishwa na mahakama ya Mwingi ulionyesha kuwa pasta Steve Musila kutoka eneo la Nguutani alimpachika mimba msichana huyo wa miaka 17 mnamo Agosti 12, 2017.

Hakimu Mkuu Mkaazi wa Mwingi mnamo Jumanne alimpa mshukiwa bondi ya Sh200,000 na mdhamini wa kiasi sawa. Jumanne, mhubiri huyo wa kanisa la Arising Christian Ministries alifika mbele ya korti kuhudhuria kikao cha kutolewa ripoti ya uchunguzi wa DNA.

Bw Masila anatuhumiwa kumnajisi mtoto huyo alipokuwa akiosha kanisa kwa maandalizi ya ibada ya Jumapili, katika siku hiyo ya Jumamosi.

Korti ilielezwa kuwa baada ya kutekeleza uovu huo, pasta huyo alimtishia mwanafunzi huyo kuwa asimwambie yeyote.

Lakini mdhulumiwa alimweleza mamake ambaye baada ya kumfikia pasta kutaka kujua ni kwanini alifanya hivyo, pasta alianza kuwatishia maisha kuwa watakufa kwa kumsingizia mtumishi wa mungu.

Pasta huyo alikana mashtaka na anazuiliwa katika jela ya Waita GK, baada ya kushindwa kugharamia bondi. Kesi hiyo inaendelea kusikizwa Septemba 18.