Pasta Ng'ang'a ajuta kutisha kumuua mwanahabari
Na ERIC WAINAINA
MHUBIRI James Maina Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism, Jumanne alishtakiwa kwa kutisha kumuua mwanahabari wa runinga ya Citizen, Linus Kaikai na kuchochea ghasia na uhasama dhidi yake.
Mhubiri huyo, ambaye alikamatwa Jumapili, alihojiwa katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.
Alishtakiwa kuhusiana na matamshi aliyotoa kufuatia kauli ya Bw Kaikai ya kulaani wahubiri wanaodanganya watu wakitumia jina la Mungu.
Bw Kaikai aliwataja wahubiri hao kama wezi: “Hawa ni wezi, sio watu wa Mungu. Hawa ni wanyonyaji katili wanaonufaika na damu ya kondoo wao wakitumia jina la Yesu. Ni watapeli ambao wanapaswa kukamatwa na polisi na kushtakiwa katika mahakama zetu,” alisema.
Baada ya Bw Ng’ang’a kuchapisha kanda hiyo, Bw Kaikai alipinga ripoti kwa polisi akilalamika kuwa alitishiwa maisha.
Kulingana na mashtaka, ilidaiwa kwamba mnamo au kabla ya Machi 10, 2019 katika Kaunti ya Nairobi, mhubiri huyo alitoa matamshi ya vitisho.
Kulingana na upande wa mashtaka, maneno hayo yalikuwa vitisho vya kumuua Bw Kaikai.
Bw Ng’ang’a, ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Kiambu Justus Kituku, alishtakiwa kwa kuchochea uhasama kwa lengo la kumdhuru Bw Kaikai.
Bw Ng’ang’a alikanusha mashtaka yote mawili na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 na mdhamini wa kiasi sawa au alipe pesa taslimu Sh200,000.
Mhubiri huyo anakabiliwa na kesi nyingine ya kusababisha kifo kwa kuendesha gari bila uangalifu.