Habari Mseto

Peter Kenneth amtaka Rais Kenyatta atangaze 'lockdown'

March 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA mbunge wa Gatanga Peter Kenneth sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta atangaze amri ya kutotoka nje kote nchini kwa wiki mbili au nne kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kenneth, ambaye pia alikuwa mgombeaji wa urais kwa tiketi ya chama cha Kenya National Congress (KNC) mnamo 2013 amesema taifa hili linaweza kudhibiti kabisa maambukizi ya virusi hivi ikiwa watu wote watalazimishwa kusalia nyumbani.

“Natoa wito na kuisihi serikali ifunge shughuli zote nchini kwa kipindi cha baina ya wiki mbili hadi nne. Kutokana na yale ambayo nimesoma na kusikia, ugojwa wa Covid-19 unaweza tu kudhibitiwa kwa kuamuru watu kutotoka nje. Tusipofanya hivyo, hatutaweza kuzuia kuenea kwa virusi hivi,” amesema Kenneth.

Kenneth amesema hayo baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza kuwa watu tisa zaidi wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona na hivyo kufikisha idadi ya maambukizi Kenya kuwa 25.

Mbunge huyo wa zamani amepongeza masharti yaliyowekwa na serikali kuzuia maambukizi lakini akawasuta baadhi ya Wakenya ambao wanakiuka maagizo hayo.