Pigo kwa KNH kumpoteza mtaalamu wa tiba ya figo
Na RICHARD MUNGUTI
Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) imepata pigo kuu baada ya mmoja wa madaktari walio na tajriba ya juu kufariki baada ya kuugua virusi vya corona.
Dkt Anthony Were, aliyekuwa mtaalamu wa tiba ya figo alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa muda wa zaidi ya wiki mbili kabla ya kuzidiwa na ugonjwa huo.
Pia alikuwa anasimamia kitengo cha matibabu ya figo katika hospitali hii kuu nchini Kenya na eneo hili la Afrika mashariki.
Katibu mkuu wa Chama cha Kutetea Haki za Madaktari (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda alitoa risala za rambirambi kwa jamii na familia ya marehemu.
Katika risala yake , Dkt Mwachonda alisema Dkt Were alikuwa mwalimu, mshauri na kiongozi mstahiki aliyekuwa amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Matibabu ya Figo Barani Afrika (AAN) na naibu wa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Figo eneo la Afrika Mashariki (EAKI).
“Siku 14 zilizopita ulikuwa umetuuliza tukuombee baada ya kulazwa tena ICU baada ya kuugua ugonjwa wa corona. Tumeamka na kupashwa habari za kusikitisha kwamba umeaga. Wewe ulikuwa mwalimu, mshauri na kiongozi wa tiba ya figo. Mungu akutunuku,” alisema Dkt Mwachonda katika risala yake kwa familia,marafiki na wafanyakazi wenzake.