• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Polisi adaiwa kuua mwanafunzi kwa kukosa kuvalia barakoa

Polisi adaiwa kuua mwanafunzi kwa kukosa kuvalia barakoa

Na SHABAN MAKOKHA

HUZUNI ilitanda Jumamosi katika kijiji cha Kajei Enyuru, Kaunti ya Busia baada ya polisi kumpiga risasi na kumuua kijana mwenye umri wa miaka 20 kwa kukosa kuvaa barakoa Ijumaa usiku.

Familia ya Victor Okiru ilishtushwa na mauaji ya Ezekiel Oduor Okiru ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuosha magari mjini Malaba.

Inadaiwa polisi waliotaka kumkamata kwa kutovaa barakoa, walimwaagiza asimame lakini akakaidi ndipo mmoja wao akampiga risasi.

Alifariki akipokea matibabu katika zahanati ya Kocholia akisubiri ambulensi ya kumpeleka katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Bungoma.

Mauaji hayo yalizua maandamano makubwa jana kwenye barabara za mji wa Malaba, waandamanaji wakitaka polisi huyo achukuliwe hatua kali za kinidhamu.

Mamake marehemu, Bi Margaret Okiru alisema mwanawe aliondoka nyumbani saa moja jioni kwenda kufunga eneo anakooshea magari na akaahidi kurejea haraka ili kushiriki chajio na familia yake.

Marehemu alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Kolanya na alikuwa akiyaosha magari ili kusaidia familia yake kujikimu wakati huu ambapo baadhi ya wanafunzi wapo nyumbani.

You can share this post!

Ripoti yadai propaganda za Rogo zilieneza ugaidi

Sonko awalilia Rais, Raila asing’atuliwe