• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Polisi akana kumlaghai mfanyabiashara Sh3.9 milioni

Polisi akana kumlaghai mfanyabiashara Sh3.9 milioni

By RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi ameshtakiwa kwa kumlaghai mfanya biashara Sh3.9milioni akisingizia atamsaidia kupewa zabuni ya kuuza madawa katika shirika la serikali la kuuza dawa (Kemsa).

Konstebo John Ochieng Gojah mwenye umri wa miaka 36 alishtakiwa pamoja na Joshua Mugiza Asava almaarufu Gabriel Asava mbele ya hakimu mkuu Bi Martha Mutuku, Mahakama ya Milimani Nairobi.

Konst Gojah na Bw Asava walikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama za kulaghai na kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu.

Mashtaka dhidi yao yalisema kati ya Mei 20 na Agosti 12 mwaka huu katika barabara ya Mombasa wakishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini walikula njama za kulaghai Bw Dominic Ongai Oloo kitita cha Sh3.9milioni wakidai watamsaidia kupewa zabuni ya kuuzia Kemsa dawa aina ya Lucentis Norvatis.

Shtaka lilisema washtakiwa hao walijua wanamdanganya Bw Oloo ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya kutengeneza sigara ya BAT na pia mkurugenzi wa kampuni ijulikanayo Magadona General Supplies.

Shtaka la pili lilikuwa la kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu. Walikana kumfuja Bw Oloo Sh3.9 wakisingizia watamsaidia kupata zabuni ya kuuzia Kemsa dawa.

Wakili Nelson Osiemo alifaulu kuwaombea dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu. Kesi itatajwa baada ya wiki mbili.

You can share this post!

Wafanyakazi wa Doshi wakana kuiba nyaya za mamilioni

Majopo 15 yaliyoundwa na Rais yavunjwa na mahakama