Habari Mseto

Polisi atolewa jasho kortini kufuatia kukamatwa kwa Gen Z

Na RUSHDIE OUDIA September 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AFISA wa polisi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Kondele mjini Kisumu alitolewa jasho alipotakiwa kueleza mahakama kwa nini iliwachukua wenzake 15 kumkamata mwandamanaji ambaye hakuwa na silaha mnamo Julai mwaka huu.

Polisi Konstebo Wilson Lawi alikuwa shahidi wa kwanza katika kesi ambapo mwanaharakati wa Kisumu Boniface Akatch anashtakiwa kwa kufunga barabara wakati wa maandamano ya kupinga serikali mnamo Julai 23, 2024, kinyume na Kifungu cha 58C cha Sheria ya Barabara ya Kenya ya 2007.

Stakabadhi za kesi zinamshutumu Bw Akatch, pamoja na wengine ambao hawakufika mahakamani, kwa kuzuia magari katika mzunguko ulio karibu na Patel Flats kwenye Barabara ya Kisumu-Kakamega.

Bw Lawi alijikanganya mara nyingi hadi akachagua kutojibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Mwenyekiti wa tawi la Kisumu la Chama cha Wanasheria Kenya, Dorcas Oluoch.