Habari Mseto

Polisi kulinda afisi za Webtribe Ltd

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

POLISI Jumatano waliagizwa wawazuilie wakurugenzi wawili wa kampuni iliyokodiwa kutoa huduma kwa hazina ya kitaifa ya bima (NHIF) kuingia katika afisi zao hadi uchunguzi ukamilishwe.

Maafisa wa polisi wameamriwa watwae ushahidi wanaotaka kabla ya kuwakubalia wawili hao kuingia kwenye afisi zao.

Kampuni ya Webtribe Ltd ijulikanayo kwa jina la Jambo Pay ilipewa kandarasi ya kukusanya pesa za wanachama wa bima ya kitaifa ya afya(NHIF).

Mabw Danson Muchemi Njunji na Robert Muriithi Muna waliamriwa wasiende katika afisi zao kwenye jengo la View Park Towers hadi maafisa wa upelelezi kutoka afisi  ya mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) wasake na kutwaa ushahidi wote utakaotumika katika kesi dhidi ya wakuu wa NHIF walioshtakiwa Jumatatu.

Hakimu mkuu Douglas Ogoti aliyeamuru wakurugenzi wasiingie katika afisi zao katika jengo la View Park . Picha/ Richard Munguti

Agizo hilo lilitolewa baada ya kiongozi wa mashtaka Bi Carol Kimiri kueleza kuwa huenda wakurugenzi wa Webtribe  Limited inayokusanya fedha kwa niaba aya NHIF wakavuruga ushahidi katika mitambo ya computer.

“ Naomba mahakama iamuru wakurugenzi wa Webtribe Ltd kuenda afisini mwao kwa vile  wataharibu ushahidi muhimu utakaotegemewa katika kesi dhidi ya wakuu wa NHIF walioshtakiwa,” alisema Bi Kimiri.

Bi Kimiri alimweleza hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti kwamba atawapelekea Mabw Mucheni na Muriithi agizo hilo la mahakama.

Kiongozi huyo wa mashtaka  alisema washtakiwa hao wawili watakubaliwa kuenda katika afisi zao baada ya ushahidi kutwaliwa na Polisi.

Bw Ogoti alitoa agizo hilo wakati wafanyakazi wawili wa NHIF Bi Millicent Wangui Mwangi na Bw David Muli Nzuki kushtakiwa kwa kashfa ya kuilaghai hazina hiyo zaidi ya Sh500 milioni.

Wafanyakazi wawili wa NHIF walioshtakiwa David Muli Nzuki na Bi Millicent Wangui Mwangi. Picha/ Richard Munguti

Bw Mutinda aliyekuwa mkaguzi wa hesabu NHIF alikanusha shtaka la kupuuza na kukaidi mamlaka ya afisi yake na kuruhusu Webtribe Ltd kulipwa Sh 179,298,575.

Bi Mwangi alishtakiwa pamoja na  aliyekuwa kinara wa NHIG Geoffrey Gitau Mwangi, Ruth Sudoi Makallah (wakili wa NHIF), Pamela Nyaboke Marendi, Gibson Kamau Muhuhu,Matilda Mwangemi na Darious Philip Mbogo kwa kutozingatia sheria za usakaji wa makampuni ya kutoa huduma.

Kampuni ya Webtribe . Mabw Njunji na Muna wameshtakiwa kwa kupokea zaidi ya Sh1.1bilioni kwa njia ya ufisadi kutoka kwa NHIF.

Bw Nzuki na Bi Mwangi walikanusha mashtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh1milioni.

Kesi itatajwa Januari 22 2019 upande wa mashtaka ueleza ikiwa umewapa washtakiwa 22 wa kashfa hiyo ya NHIF nakala za mashahidi.