Polisi waamriwa kumrudishia mganga wa Kangundo magari yake matano
Na RICHARD MUNGUTI
MKURUGENZI wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) ameamriwa amrudishie mganga maarufu wa Kangundo, kaunti ya Machakos Bi Annah Mutheu Ndunda magari matano yaliyonaswa kutoka nyumbani kwake.
Hakimu mwandamizi Bi Electer Riany alimtaka afisa wa polisi Konstebo James Mwangi wa afisi ya DCI kitengo cha uchunguzi wa jinai amrudishie Bi Ndunda magari hayo pamoja na hati za usajili.
Bi Riany alitoa agizo hilo baada ya wakili anayemtetea Bi Ndunda kuomba magari hayo yaachiliwe kwa vile Polisi hawakumpata na hatia ya kumshtaki mshukiwa huyo kwa hatia yoyote.
Akasema Bi Riany katika uamuzi wake, “Baada ya kusikiza ombi la Bi Ndunda kupitia kwa wakili wake naamuru Konstebo Mwangi wa afisi ta DCI amrudishie mlalamishi magari matano yaliyotwaliwa kuchunguzwa.”
Hakimu aliyataja magari hayo kuwa KCL 425M Toyota Hilux, KBT 283-Toyota Hilux, KBM 066R-Toyota Hilux, KBM 397J-Isuzu Lori na KAH 311U- Toyota Matatu.
Agizo lilitolewa baada ya polisi kusema hawajapata ushahidi wowote kumfungulia mashtaka yoyote mshukiwa huyo.
Bi Ndunda alikuwa ametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki katika visa vya wizi wa magari na visa vya uhalifu.
Bi Rianyi alimwachilia Mutheu baada ya afisa wa polisi aliyekuwa anachunguza kesi hiyo kusema “hakupata ushahidi wa kutosha kuweza kumfungulia mashtaka mshukiwa huyo.”
Mutheu alitiwa nguvuni mnamo Oktoba 9 2018 pamoja na Bw John Macharia Kiragu.
Maafisa wa Polisi wa kitengo cha kupambana na uhalifu almaarufu Flying Squad (FS) walimtia nguvuni Mutheu na kumsafirisha kutoka Tala kaunti ndogo ya Kangundo kaunti ya Machakos.
Alisafirishwa hadi makao makuu ya FS kumchunguza ikiwa alikuwa anashiriki katika uhalifu baada ya polisi kupata magari matano ikiwamo Lori.
Mbali na magari hayo muundo wa Toyota na Isuzu Mutheu alikutwa na vitambulisho vya kitaifa 112.
Afisa aliyekuwa anachunguza kesi hiyo Konstebo James Mwangi alimfikisha Mutheu na Bw Kiragu mbele ya Bi Rianyi na kuomba aamuru wazuiliwe kwa muda wa siku 10 ndipo akamilishe uchunguzi.
“Naomba hii mahakama iamuru washukiwa hawa wazuiliwe katika kituo cha polisi kuhojiwa na kuwasaidia Polisi kuchunguza iwapo magari yaliyokutwa katika makazi ya Mutheu yameibwa ama yameripotiwa kupotea,” alisema Konstebo Bw Mwangi Oktoba 9 2018.
Pia alieleza korti kuwa anataka kuwasiliana na idara ya usajili wa magari na mamlaka ya uchukuzi NTSA kubaini wenye magari hayo.
Afisa huyo pia alimweleza hakimu kuwa atachunguza vitambulisho hivyo kuwatambua wenyewe katika idara ya usajili wa watu.
Pia polisi walikuwa wanachunguza vitambulisho hivyo kubaini ikiwa ni halisi.
Mutheu na Kiragu walipinga wakizuiliwa kwa muda wa siku 10 na kuomba waachiliwe kwa dhamana.
Bi Rianyi aliwaacha kwa dhamana ya Sh150,000.
Jana Bi Rianyi alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Adeline Rugoto ikiwa uchunguzi umekamilishwa.
“Uchunguzi katika kesi hii umekamilishwa?” Bi Rianyi alimhoji Bi Rugoto.
“Polisi wamekamilisha uchunguzi lakini hawakupata ushahidi wa kutosha kuwawezesha kumfungulia mashtaka Mutheu na Kiragu,” alisema Bi Rugoto.
Aliomba hakimu awaachilie Mutheu na Kiragu kwa kutopatikana na ushahidi wa kuwezesha polisi kuwafungulia mashtaka.
“Kesi dhidi yenu imefungwa. Mmeachiliwa. Mutheu atarudishiwa dhamana ya Sh150,000 pesa tasilimu aliyokuwa amelipa kortini,” aliamuru Bi Rianyi.
Mutheu na Kiragu waliondoka mahakamani wakiwa huru.
Mutheu alijipatia umaarufu kwa kuwafanya watu waliotekeleza uhalifu kukamatwa na walalamishi ama kurudisha mali waliyodaiwa wameiba.