Habari Mseto

Polisi waua washukiwa 2 waliokuwa wakiuza risasi

March 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA OSCAR KAKAI

Washukiwa wawili Jumamosi waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi eneo la Kitalakapel kwenye barabara ya Makutano –Kacheliba, Kaunti ya Pokot Magharibi wakijihusisha na biashara za kuuza risasi kutoka nchi jirani ya Uganda.

Zaidi ya risasi 1,850 za milimita 7.65 zilipatikana kutoka kwa washukiwa.

Wawili hao ambao walitambuliwa kama Lonyang Kareng 29 na Kopounyang Achom Picot 42, walipigwa risasi baada ya maafisa wa upelelezi kupashwa habari na raia kuhusu watu waliokuwa wakijihusisha na biashara ya kuuza silaha haramu.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda ya polisi katika kaunti hiyo Bw Mathew Kuto alisema kuwa maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa kwenye makabiliano makali kati ya majangili hao na polisi.

“Polisi waliarifiwa na kuanza kufanya msako kwenye barabara hiyo. Baada ya muda mfupi, washukiwa waliwasili wakiwa kwenye pikipiki na walipoona maafisa wa polisi walianza kuhepa. Polisi waliwafuata na kuwaua. Polisi walipata risasi kwenye mkoba ambao washukiwa walikuwa nao,” alisema Bw Kuto.

Alisema kuwa vitambulisho vya wahalifu hao vinaonyesha kuwa wote ni wenyeji wa Kaunti ya Pokot Magharibi.

Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa maafisa wa polisi katika kaunti hiyo wameimarisha msako na wako chonjo kushika washukiwa ambao wanajihusisha na biashara za kuuza silaha haramu na risasi.

Bw Kuto alitoa wito kwa wakazi kutambua na kupiga ripoti kuhusu wahalifu.

Alisema kuwa kuuza kwa silaha haramu na risasi kunachangia visa vingi vya uvamizi na wizi wa mifugo katika eneo hilo. Miili za washukiwa hao ilipelekwa katika mochari ya Kapenguria kufanyiwa upasuaji .