Habari Mseto

Polisi wazima mkutano Bomet kujadili Mau

November 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na VITALIS KIMUTAI

USALAMA uliimarishwa Jumamosi mjini Bomet baada ya polisi kupiga marufuku mkutano uliopangwa na wanasiasa mbalimbali wa Bonde la Ufa kuzungumzia hatima ya familia zilizohamishwa kutoka msitu wa Mau.

Polisi wenye silaha na waliovaa maalum kukabiliana na ghasia walifunga uwanja wa Bomet Green Stadium ambapo mkutano huo ulipangwa kufanyika jana, lakini ukatibuka baada ya kamati ya usalama ya kaunti kufuta kibali ilichokuwa imewapa waandalizi Jumatatu iliyopita.

Magavana kutoka Bonde la Ufa, wabunge, madiwani, wanasiasa wengine na viongozi wa kidini walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Ilitarajiwa kuwa viongozi hao wangetumia hafla hiyo kushinikiza serikali kusitisha mipango ya ufurushaji wa familia hizo zinazoishi maeneo ya msitu wa Mau.

Mwenyekiti wa Chama cha wanasheria tawi la Kusini mwa Bonde la Ufa, Kipngetich Korir na mwanaharakati Tyson Ngetich waliokuwa wameomba kibali hicho, walishutumu serikali kwa kukiuka haki ya kukusanyika pamoja na kujieleza.

Sababu

“Mkutano ulifutiliwa mbali kutokana na sababu za kiusalama na kuruhusu wanafunzi kufanya mtihani wa kidato cha nne (KCSE) bila vurugu zozote. Tumewasiliana rasmi na watu walioomba kibali,” alisema Kamishna wa Kaunti hiyo Geoffrey Omoding.

Bw Omoding alisema: “Hatungeruhusu viongozi na wanaharakati wa kisiasa kutoka maeneo mengine kuja kuvuruga amani na utangamano uliopo katika kaunti hii. Ufurushaji watu msituni unafanyika katika kaunti jirani na wala si katika eneo letu.”

“Kuhusu masuala ya usalama, hatuchukulii chochote kwa urahisi. Ni haki ya watu kushiriki mikutano lakini usalama wao na wa wengine unapewa kipaumbele,” alisema Bw Omoding.

Akiandamana na Kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo Naomi Ichami, Mkuu wa upelelezi wa Jinai katika Kaunti hiyo Jacob Muli na wanachama wa kamati ya usalama katika kaunti, Bw Omoding aliongoza maombi katika mkutano wa asubuhi ulioandaliwa Gavana Barchok.