Profesa Hamo aongoza hamasisho la kulinda vifaru
RICHARD MAOSI NA MAGDALENE WANJA
MAKALA ya 15 ya waendeshaji baiskeli katika Kaunti ya Nakuru kuhusu uhamasisho wa kulinda wanyamapori yaliandaliwa Jumamosi katika Mbuga ya Nakuru.
Hamasisho hili lililenga kuhimiza jamii umuhimu wa kulinda vifaru weusi mbugani dhidi ya majangili walioshika kasi kuwaangamiza.
Wanafunzi kutoka shule za msingi na upili waliendesha baiskeli ndani ya mbuga huku maafisa wa kitengo cha usalama wa wanyama pori wakitoa ulinzi mkali.
Victoria Wanjiru (11) alisema hii ni mara yake ya nne kushiriki mashindano haya, na ameshuhudia idadi kubwa ya washiriki ikiongezeka kila mwaka. Anasema ilikuwa fahari kuendesha baiskeli katikati ya pundamilia, twiga na vifaru.
Mchekeshaji Herman Kago almaarufu kama Professa Hamo katika kipindi cha runinga ya NTV cha Churchill Show, ambaye ni balozi wa vifaru katika mbuga ya Nakuru aliongoza hafla hiyo iliyovutia maelfu ya washiriki.
“Mwaka huu idadi ya washiriki ni nzuri sana kuliko miaka ya nyuma, na tunaamini hali hii itaendelea na iwe kubwa zaidi katika awamu ya 16, ifikapo mwaka ujao,” Hamo alisema.
Azma kubwa ya mashindano haya ikiwa ni kuwahimiza wanafunzi kuzingatia umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa vizazi vijavyo,hasa raslimali za halisia.
‘’Kizazi cha kesho kina mchango wake katika mazingira ,iwapo watoto watafundishwa tija inayotokana ya mimea na wanyama wanaweza kuyasimamia vyema,’’ aliongeza Profesa Hamo.
Mkurugenzi wa utalii Profesa Charles Musyoki alisema mwaka uliopita ni shule 11 zilizoshiriki,kinyume na Jumamosi ambapo idadi imeongezeka hadi 24.
Kaunti ya Nakuru, Kisumu na eneo la Gilgil likiwakilishwa. “Zaidi hii inaonyesha uzalendo wa viongozi wa kesho kwa taifa lao,” Bw Musyoki alisema .
Japo eneo kubwa la kilomita 20 mraba lilizama kutokana na mafuriko ya kila mwaka, bado wakazi wa hapa wanazidi kupatia mbuga hii hadhi yake kwa kupiga jeki utaliiwanapozuru mbuga yenyewe.
Mbuga ya Nakuru inapatikana mjini hivyo basi inakumbana na changamoto nyingi za uchafuzi wa mazingira kutoka kwenye viwanda vilivyojaa taka.
Mbuga ya Nakuru ilikuwa kivutio cha ndege mnamo 1961 na hatimaye hekta 6000 yaani kilomita 64 mraba ikaongezwa ili kuhifadhi idadi Zaidi ya wanyama pori. Baadaye 1968 ilifanywa mbuga ya kitaifa.
Ilipanuliwa hadi kilomita 188 mraba mnamo 1974 ukubwa wa mbuga hiyo hadi sasa kupitia udhamini wa World Wide Fund(WWF),kutokana na mchango wake duniani katika utalii.
Mwaka 1984 ilifanywa mbuga rasmi ya kulinda vifaru wa aina zote,baadaye 1987 ikapandishwa kuwa mojawapo ya kivutio cha chemichemi kupitia mkataba na UNESCO miongoni mwa Bogoria na Elementaita katika bonde la ufa.