Puuzeni uvumi kwamba Matiang'i amelazwa hospitalini – Serikali
Na CHARLES WASONGA
WIZARA ya Masuala ya Ndani Ijumaa, Julai 24 ilipuuzilia mbali habari zinazosambazwa mitandaoni kwamba waziri Fred Matiang’i amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.
Kwenye taarifa fupi katika akaunti yake ya Twitter, wizara hiyo ilitaka umma kuchukulia habari hizo kama za uwongo.
“Wananchi wanashauriwa kupuuzilia mbali habari feki na za kupotosha zinazosambazwa katika mitandao mbalimbali kwamba Waziri Dkt Fred Matiang’i amelazwa hospitalini. Madai hayo sio ya kweli hata kidogo,” taarifa hiyo ikasema.
Hata hivyo, wizara hiyo haikutoa maelezo kuhusu aliko Waziri Matiang’I kwa sababu hajaonekana hadharani tangu Julai 16. Hii ni licha ya kwamba huyu ni Waziri ambaye amekuwa akionekana hadhara kila mara na hata kutumia jumbe nyingi katika mitandao ya kijamii.
Taarifa zimekuwa zikisambazwa mitandaoni kuanzia Alhamisi jioni na Ijumaa zikidai kuwa Waziri Matiang’I amelazwa hospitalini.
Na mapema wiki hii gazeti la The Standard liliripoti kuwa mawaziri wawili na afisa mmoja wa cheo cha juu katika serikali ya kitaifa wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona.
Watatu hao ilisemekana walishauri kujitenga nyumbani, na watunzwe, huko kulingana na mwongozo wa Wizara ya Afya, kwa sababu hawakuwa wameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Mnamo Julai 21, Rais Uhuru Kenyatta aliwazima mawaziri wote kusafiri nje ya Nairobi kama hatua ya kupunguza uwezekano wa wao kuambukizwa virusi vya corona.
Hii ni kufuatia kugunduliwa kwa visa vya maambukizi ya Covid-19 miongoni mwa wafanayakazi wa wizara mbalimbali za serikali kuu. Hali hiyo ilipelekea kusitishwa kwa baadhi ya huduma muhimu katika baadhi ya Wizara na Idara za Serikali Kuu
“Unashauria kutoondoka Nairobi kwa muda wa wiki moja ijayo. Amri hii inaanza kutekelezwa kuanzia leo (Julai 21),” taarifa hiyo ya Rais Kenyatta ikasema.