Habari Mseto

Rabsha kwenye mazishi Kirinyaga Askofu alipojaribu kuzuia wandani wa Gachagua

Na GEORGE MUNENE March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RABSHA zilitokea Jumanne katika Kaunti ya Kirinyaga Askofu mmoja na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti hiyo Njeri Maina waliporushiana cheche za maneno wakati wa ibada ya wafu ya watoto watatu waliokufa katika ajali ya pikipiki.

Hatimaye Askofu Simon Munene wa Kanisa la Full Gospel alilazimika kutoroka kutoka uwanja wa Shule ya Msingi ya Kimunye katika eneo bunge la Gichugu alipokabiliwa na waombolezaji wenye hamaki.

Waombolezaji hao walikasirishwa na tangazo la Askofu huyo aliyetarajiwa kuongoza ibada hiyo kumwonya Bi Maina kwamba asingeruhusiwa kuchapa siasa.

Alimkumbusha kuwa hiyo ilikuwa ni ibada ya wafu wala si mkutano wa kisiasa na kumshauri kwamba angeruhusiwa tu kutoa risala za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Hata hivyo, Bi Maina alimrushia maneno makali Askofu huyo akimshutumu kwa kuwazuia wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kunena ukweli kuhusu yanayotendeka nchini.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa wakazi wa eneo hilo na Wakenya kwa ujumla sharti waelezwe ukweli kuhusu changamoto zinazolikumba taifa ukiwemo udhaifu wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).

Wakati mmoja Askofu Munene alielekea jukwaani na kumnyang’anya Bi Maina kipaza sauti, kitendo kilichopingwa kabisa na waombolezaji.

“Hii ni ibada ya wafu wala sio mkutano wa kisiasa!” akamwambia Mbunge huyo Mwakilishi wa Kaunti ya Kirinyaga.

Hii iliwakasirisha waombolezaji waliosimama na kuapa kwamba ibada hiyo isingeendelea hadi pale Bi Maina na wanasiasa wengine waruhusiwe kuhutubu.

Ghafla bin vuu, baadhi ya waomboleza walianza kurusha viti vya plastiki, wengine wakipiga mayowe huku wengi wakisonga karibu na jukwaa wakisisitiza kuwa Bi Maina na viongozi wengine sharti waruhusiwe kuwahutubia.

Walimpigia kelele Askofu huyo na kuvuruga ibada kwa muda. Juhudi za idadi ndogo ya maafisa wa polisi waliokuwa hapo kutuliza hali hazikufua dafu huku baadhi ya waombolezaji wakiamua kuchana mbuga.

Baada ya kung’amua kuwa maisha yake yalikuwa hatarini Askofu Munene aliondoka haraka mahala hapo huku akifuatwa unyo unyo na waombolezaji.

“Siwezi kuwahubiria watu wanaopiga mayowe. Nawezaje kuhubiri neno la Mungu wakati genge la wahuni waliokodiwa wanapiga kelele,” akasema na huku akiondoka kwa gari lake.

Baadaye, ibada ilirejelewa na Bi Maina akawahutubia waombolezaji huku wakimshangilia.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, Mbunge wa Gichugu Gichimu Githinji na Diwani wa wadi ya Baragwi David Mathenge.

Bw Githinji, ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto, alipewa fursa ya kuhutubu, alizomewa huku waombolezaji wakikataa risala za rambirambi alizowasilisha kutoka kwa Rais na Naibu wake Kithure Kindiki.

Hata hivyo, Seneta Murango, ambaye ni mwandani wa Gachagua, alishangiliwa.

Ibada hiyo ilikuwa ni ya kuwakumbuka watoto; Kelvin Mugambi, 17, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Upili ya Kimunye Forest, na Morris Muriithi, 14 na Fidelious Ng’ang’a 15 ambaye ni wanafunzi wa Gredi ya 9 katika Shule ya Msingi ya Kimunye waliokufa Februari 23 wakiendesha pikipiki.