Raia wa Amerika kutuliza hasira gerezani
Na RICHARD MUNGUTI
RAIA wa Amerika aliyemchapa na kumsababishia majeraha afisa wa polisi katika hoteli ya Azuri baada ya kukatazwa kuingia lojing’i akiandamana na msichana amezuiliwa katika gereza la Eneo la Viwandani kwa muda wa siku sita.
“Ninaomba hii mahakama iamuru mshukiwa huyu Alex Harpe azuiliwe katika gereza la Viwandani. Atawavuruga mashahidi; atatoroka akiachiliwa kwa dhamana. Yeye ni raia wa Amerika na hafai kuachiliwa kwa dhamana kwa vile hana makazi maalum nchini,” kiongozi wa mashtaka James Gachoka alimweleza hakimu mwandamizi Bi Hellen Onkwani.
Bi Onkwani alifahamishwa kwamba mshukiwa huyu alipandwa na mori Oktoba 14, 2019, katika hoteli ya Azuri iliyoko Kileleshwa na kumfukuza afisa wa mapokezi alipoelezwa ni sheria ya hoteli kwamba “wanaume hawaruhusiwi kuingia hotelini pamoja na wasichana.”
Huku akiona uhondo aliotazamia kupata umekatizwa, raia huyo wa Amerika, imeelezwsa alipandwa na mori ndipo akaanza kuwashambulia wahudumu wa hoteli na kumtimua mbio kutoka sebuleni afisa wa mapokezi.
Mawakili Felix Kiprono, Festus Mbati, Francis Karanja na Bw Gachoka walimsihi hakimu “amzuilie Harpe kwa vile ni hatari kwa usalama.”
Mahakama ilielezwa Koplo Duncan Kiprono aliyepigwa na kujeruhiwa alikuwa amejihami kwa bastola lakini alijizuia kumfyatua risasi mshtakiwa kwa sababu anathamini maisha ya binadamu.
“Koplo Kiprono alijizuia tu licha ya kuchapwa kama mchunga kondoo asiye na ufahamu licha ya kuwa mjuzi wa matumizi ya silaha,” alisema wakili Kiprono.
Lakini mshtakiwa kupitia kwa wakili wake aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “Katiba imeipa mahakama mamlaka na nguvu ya kumwachilia kwa dhamana.”
Mahakama ilifahamishwa kuwa mshtakiwa hawezi kutoroka kwa vile yuko na kampuni kubwa katika uwanja wa ndege wa Wilson na “ hawezi kutoroka kuacha rasilmali zake.”
Akitoa uamuzi, hakimu aliagiza mshtakiwa (Harpe) azuiliwe katika gereza la Viwandani kutuliza hasira kwa siku sita kabla ya uamuzi wa ombi la dhamana kutolewa.