Habari Mseto

Raia wa Amerika wafunga ndoa ya Kipokot

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WANANDOA wawili ambao ni raia wa Amerika wamefanya harusi ya kitamaduni ya jamii Pokot.

Bi Teresa na Bw Tony walisema walichukua hatua hiyo baada ya kuzuzuliwa na utamaduni w jamii ya Pokot baada ya kuisha na wao kwa mwongo mmoja.

Wawili hao wamekuwa wakiishi katika eneo la Chepangus, eneobunge la Taity, Kaunti ya Baringo ambako wamekuwa wakiendesha kazi ya Kimishenari.

Harusi hiyo ya kufana ilifanyika katika milima ya Paka Hills katika eneobunge hilo linalowakilishwa bungeni na William Kamket.

“Nina furaha kubwa kuwa hapa na kushiriki katika hafla hii. Ni baraka kwangu kuandaa harusi hii na kukubalika na wakazi wa eneo hili,” Tony aliwaambia wanahabari Jumamosi.

Baada ya sherehe hiyo, Bi Harusi, Teresa alipewa jina la Kipokot, Cheigar.

Wakazi wafurahia

Wakazi wa eneo hilo walisema wamewakubali wanandoa hao na kuchangamkia hatua ya wao kukumbatia utamaduni wao.

“Tumefurahi sana kwa sababu hawa ndio wageni wa kwanza kuja hapa kutusaidia katika masuala mbalimbali. Hii ndio maana tumewapa majina ya hapa kwetu,” mkazi mmoja alisema.

Bwana harusi, Tony, alielezea namna ambavyo alilipa mahari kufungamana na mila na tamaduni za jamii ya Pokot.

“Nimelipa ngamia, mbuzi kadhaa, chakula, vinywaji na pesa kama mahari yote inayohitajika kufungamana na tamaduni ya Pokot, ” akasema.

Sherehe hiyo ilikamilika katika nyumba ya kitamaduni ya bwana harusi ambapo wawili hao walitambuliwa rasmi kama mume na mke kufungamana na utamaduni ya jamii ya Pokot.